1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la seneti launga mkono mkataba wa START

Sekione Kitojo22 Desemba 2010

Uidhinishaji wa mkataba wa START kati ya Marekani na Urusi unakaribia kukamilika, baada ya baraza la seneti kukamilisha mjadala na leo utapigiwa kura.

https://p.dw.com/p/zoFc
Rais Barack Obama, anamatumaini kuwa mkataba wa START utaidhinishwa katika siku mbili zijazo.Picha: AP

Kuidhinishwa kwa mkataba maalum kati ya Marekani na Urusi kuhusu upunguzaji wa silaha za kinuklia unakaribia kukamilika. Kwa kura 67 za ndio dhidi ya 28 , baraza la seneti la Marekani liliidhinisha jana hatua ya mwisho ya kuufikisha mwisho mjadala kuhusu mkataba huo. Ikulu ya Marekani White House inaona kuwa hii ni hatua muhimu katika kuuidhinisha mkataba huo , mkataba ambao wabunge wa chama cha upinzani cha Republican ambao wamekuwa kwa muda wa siku kadha wakipinga wakipendelea kuuendeleza mjadala huo kwa nia ya kuuchelewesha. Lakini wabunge kadha wa chama hicho cha Republican wameweza kuunga mkono mjadala kuhusu mkataba huo wakijiunga na wabunge wa chama cha Democratic . Kura kamili ya kuidhinisha hata hivyo itafanyika leo Jumatano.

Upinzani wa wabunge wa chama cha Republican dhidi ya mkataba huo wa START, uliporomoka kutokana na kwamba uidhinishaji mkataba huo wa kupunguza silaha ulikuwa na mbinyo mkali. Mawaziri wote wa kutoka chama cha Republican ambao waliwahi kuwa katika wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni, waziri wa ulinzi Robert Gates na mwenyekiti wa jopo la wanadhimu wakuu wa jeshi Mike Mullen kwa pamoja wamesema kuwa mkataba huo ni lazima uidhinishwe kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Katika mkutano wa jumuiya ya NATO mjini Lisbon mataifa kadha ya Ulaya kuanzia Lithuania na Norway, kutoka Denmark hadi Hangary na Bulgaria wamekubali wazo la kuwa na mkataba kama huo. Hata kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameeleza kuwa anamatumaini mkataba wa START utaidhinishwa.

Rais Obama Jumamosi iliyopita alitumia hotuba yake ya kila wiki kwa njia ya radio kuzungumzia kuhusu mkataba huo wa START, na kusisitiza juu ya umuhimu wake.

"Bila ya kuwa na mkataba kama huu tunahatarisha kurejesha nyuma hatua zilizopigwa katika ushirikiano wetu na Urusi. Ushirikiano ambao ni muhimu katika kutekeleza vikwazo imara dhidi ya Iran, kulinda mada muhimu za kinuklia dhidi ya magaidi, na kupeleka misaada muhimu kwa vikosi vyetu nchini Afghanistan".

Maseneta wa chama cha Republican hawakutaka kuzuwia uamuzi huo kama walivyofanya katika baraza la zamani, wakati huu ambapo kwa kura za wabunge wa chama hicho kutapatikana wingi wa kuidhinisha mkataba huo. Baraza la Seneti linapaswa kuupitisha mkataba huo kwa wingi wa theluthi mbili, ikiwa ni kura 67 , iwapo maseneta wote 100 watakuwapo katika upigaji kura. Kuanzia Januari kura 14 za Warepublican zitakuwa ni muhimu, kwa sababu katika uchaguzi wa baraza la Congress mwezi Novemba mwaka huu Warepublican walipata viti zaidi katika baraza la seneti.

Mkataba wa START ulitiwa saini tarehe 8 Aprili mwaka huu na rais Barack Obama pamoja na mwenzake wa Urusi Dimitry Medvedev. Mkataba huo unataka kupunguzwa kwa makombora ya kinuklia kufikia kiwango cha 1550 katika pande zote mbili. Idadi ya mifumo ya kufyatulia makombora hayo , nyambizi pamoja na ndege za kivita vinapunguzwa kwa kila nchi na kufikia 800 tu.

Mwandishi : Bergmann, Christina / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri: Abdul-Rahman