1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bangakok yakaribia kuzama

25 Oktoba 2011

Serikali ya Thailand imewapa wafanyakazi siku tano za likizo ili waweze kuuhama mji mkuu wa Bangkok na kukimbilia maeneo salama, katika wakati ambao mafuriko yanaukumba mji huo kwa kasi isiyoweza kuzuilika.

https://p.dw.com/p/12yJw
Wakaazi wa jimbo la Nonthaburi wakijaribu kujiokoa kutokana na mafuriko.
Wakaazi wa jimbo la Nonthaburi wakijaribu kujiokoa kutokana na mafuriko.Picha: AP

Picha halisi ya Bangkok ni ya mji unaozama. Kiasi ya wakaazi 30,000 wa kaskazini mwa mji huo wametakiwa kuyahama makazi yao baada ya uzio uliowekwa kwenye mto Raphipat, unaotenganisha mji uliokwishaghariki wa Ayutthaya na Bangkok, ukiripotiwa kuvunjika.

Jeshi limepeleka magari ya kuwasaidia watu kukimbia maeneo yaliyo hatarini kuzama kabisa. Wale walio upande wa kusini watavamiwa na maji yaendayo kwa kasi yenye kina cha mita 1 hadi 1.5, kwa mujibu wa mkuu wa polisi Pracha Promok, ambaye ndiye mkurugenzi wa kituo cha operesheni ya uokozi kwenye janga hili. Inaonekana kwamba hakuna kitakachosalimika na maji haya.

"Maji yameifunika kabisa nyumba yetu, hadi ghorofa ya pili, na pia yameiziba njia ya kutokea nje." Amesema Onnut Bapa, mkaazi wa Patumthami, ambaye binafsi ameshapoteza kila kitu

Kituo cha operesheni ya uokozi kinawalaumu wakaazi wa Ayutthaya, uliokuwa mji mkuu wa zamani wa Thailand, kwa kuubomoa uzio, lakini wakaazi hao wanauona uzio huo kuwa ulikusudiwa kuunusuru mji wa Bangkok kwa gharama ya kughariki kwa mji wao.

Viwanja vya ndege vyafungwa

Wakaazi wa jimbo la Phatum Thani wakivuuka mkondo wa maji ya mafuriko.
Wakaazi wa jimbo la Phatum Thani wakivuuka mkondo wa maji ya mafuriko.Picha: AP

Maji haya pia sasa yameufikia uwanja wa ndege wa Don Muang, ambao ni wa pili kwa ukubwa mjini Bangkok, na kulazimisha kusitishwa kwa safari za ndege.

Mkuu wa Shirika la Ndege la Nok Air, Patee Sarasin, ameliambia Shirika la Habari la Associated Press, kwamba wanasitisha huduma zao hadi tarehe 1 Novemba kwa sababu maji yameingia sehemu ya kaskazini ya uwanja huo wa ndege.

Sasa huduma za Nok Air na za shirika jengine la Orient Thai Airlines, zitaelekezwa katika uwanja wa ndege mdogo wa Suvarnabhuni.

Mafuriko haya yamelazimisha pia kufungwa kwa viwanda saba katika majimbo ya Ayutthaya, Nonthaburi na Pathum Thani, ambayo yote yanauzunguka mji mkuu wa Bangkok. Miongoni mwa makampuni yaliyofunga viwanda vyake ni ile ya magari ya Japan, Toyota, na ya vifaa vya kielektroniki, Sony na Nikon.

Kufungwa kwa viwanda hivyo kumesababisha hasara ya dola bilioni 3.2 hadi sasa, kumeharibu mfumo wa usambazaji bidhaa na kumewakosesha kazi kwa muda wafanyakazi 650,000.

Serikali yatangaza bajeti ya fidia

Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra.
Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck Shinawatra.Picha: dapd

Hivi leo, serikali imetangaza bajeti ya dola bilioni 7.3 kuvifidia viwanda hivyo mara ya mafuriko kumalizika, lakini si wazi hadi sasa hasara zinazowapata watu wa kawaida, wakiwemo watoto wadogo, wanafunzi, na masikini waliokwishapoteza kila kitu, zitafidiwa vipi.

"Tuna kiasi ya watu 2,500 hapa, familia kadhaa zikiwa na watoto wao, na watoto hawa wanahitaji kufanyiwa kitu ili mkasa huu usiwaumize akili zao." Amesema Seven Nouk, mmoja wa wafanyakazi wa kujitolea kwenye kituo cha kuwafaraiji waathirika wa mafuriko haya.

Bado haijafahamika hatima ya mafuriko haya, lakini kwa vyovyote hasara yake ni kubwa. Kisiasa, janga hili la kimaumbile umekuwa mtihani wa kwanza kwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke, Yingluck Shinawatra, ambaye hadi sasa analaumiwa na wakosoaji wake kwa kutokuwa na uwezo wa kukabili matatizo makubwa kama haya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji