1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Bahati nzuri kwa siasa"

Maja Dreyer18 Juni 2007

Matukio ya wikiendi yalikuwa mengi, sawa na masuala yanayozingatiwa na wahiriri wa magazeti leo hii.

https://p.dw.com/p/CHSg

Tuanze na hali katika maeneo ya Wapalestina ambako serikali mpya imeapishwa, wakati eneo la Gaza linathibitiwa na kundi la Hamas. Kulingana na “Frankfurter Allgemeine Zeitung” kuna faida fulani yaani:

“Tangu kundi la Hamas lenye msimamo mkali wa Kiislamu linadhibiti utawala wa ukanda wa Gaza, angalau hali ni wazi. Kwa kutumia nguvu, Hamas imetekeleza ushindi wake kwenye uchaguzi wa mwaka 2006. Sasa inabidi ionyeshe uwezo wake wa kutawala vizuri.”

Mhariri wa “Financial Times Deutschland” anaichambua hivi hali ya Palestina:

“Licha ya idadi kubwa ya watu waliouawa, rais Abbas ametumia muda mfupi tu kuimarisha upya wadhifa wake. Hamas, kwa upande wake katika eneo la ukanda wa Gaza, ina mpango wa kuweka taifa la kidini kama lile la Iran. Huenda Israel itatumia mgawanyiko kati ya Wapalestina kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Hamas.

Ni gazeti la “Financial Times Deutschland”. Tuelekee Ufaransa sasa, ambako chama cha Kihafidhina chini ya rais mpya Nicolas Sarkozy kimeshindwa kupata theluthi mbili za viti vya bunge. Ufuatayo ni uchambuzi wa gazeti la “Berliner Zeitung”:

“Baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge, chama cha Kihafidhina kilitarajiwa kushinda kwa uwingi mkubwa, lakini katika duru hii ya pili hakikufaulu kufikia lengo hili. Sababu ya kura zake kupungua ni taarifa ya rais Sarkozy aliyetangaza mpango wake wa kuongeza kodi ya mauzo ili aweze kupungua gharama za kuwaajiri watu na hivyo kupata nafasi zaidi za kazi. Bado lakini, rais huyu anaweza kutekeleza mageuzi yake akiwa na wingi katika bunge.”

Gazeti la “Neue Osnabrücker” halifichi furaha zake juu ya matokeo ya uchaguzi wa Ufaransa. Limeandika:

“Kwa bahati nzuri, Wafaransa jana walikuwa na busara katika duru ya pili ya uchaguzi wa bunge na kuzuia uwingi wa theluthi mbili wa chama kimoja. Ni faida kubwa kwa siasa na fursa za kujadiliana bungeni.”

Na katika suala la pili tunabakia barani Ulaya. Siku chache kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, mazungumzo juu ya mageuzi katika Umoja huu na kupitisha katiba yamekwama. Nchi inayomzuia Kansela Merkel wa Ujerumani katika juhudi hizo ni Poland na ndiyo maana, wahariri wengi wanaikosoa serikali ya Poland. Hili hapa gazeti la “Dresdner Neueste Nachrichten”:

“Kabla ya mkutano wa baadaye wiki hii, Kansela Angela Merkel alijipatia uungwaji mkono kutoka nchi karibu zote wanachama wa Umoja wa Ulaya – ila tu jirani wa Ujerumani upande wa Mashariki, yaani Poland. Hilo ni jambo lisiloweza kufahamika, kwani Ujerumani iliisaidia sana Poland kukubaliwa kuingizwa katika Umoja huu. Haya yanaonyesha kwamba shukrani katika siasa hazina umuhimu tena.”