1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD:Spika afurushwa bungeni

11 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBsg

Bunge nchini Iraq limemfurusha Spika wake Mahmud Mashhadani baada ya kudaiwa kuwaagiza walinzi wake kumvamia mbunge mmoja wa Kishia.Hayo ni kwa mujibu wa naibu wa Spika.Wabunge 113 walipiga kura iliyoidhinisha kufukuzwa kazini kwa Spika huyo.Bunge limelipa muungano wa National Concord Front unaowakilisha waSunni wengi wiki moja kuchagua mgombea mwingine kwa wadhifa huo

Bwana Mashhadani anayejulikana kwa kauli zake kali bungeni aliwaagiza walinzi wake kumvamia Fariyad Mohammed jumapili iliyopita baada ya majibizano makali kati yake na walinzi hao.

Hilo lilikuwa tukio la pili lililomuhusisha spika huyo wa zamani.

Mapema mwaka huu Bwana Mashhadani alimzaba kibao mbunge mwenzake Hussein Falluji karibu na mkahawa wa bunge kufuatia majibizako makali. Mashhadani ni mfuasi wa dini ya kale katika shule ya Salafi aliyehukumiwa kifo wakati wa utawala wa Saddam Hussein iliyobadilishwa kuwa kifungo cha miaka 15 mwaka 200.Inadaiwa kuwa alimhonga jaji ili kubadilishiwa hukumu hiyo.

Bunge la Iraq limezongwa na wabunge wanaotoa kauli kali hasa wa Kishia wanaolalamika mara kwa mara kuwa wanatengwa na serikali vilevile katika shughuli za kuendesha serikali.

Wakati huohuo waziri mkuu mtarajiwa wa Uingereza Gordon Brown yuko ziarani nchini Iraq ili kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki.Bwana Brown na Waziri Mkuu wa Uingereza anayeondoka Tony Blair wanashinikizwa na waingereza kwa kuhusika katika vita vya Iraq vilivyodumu miaka mine na kusababisha vifo vya wanajeshi 150 wa Uingereza.Wabunge wa chama cha upinzani cha Conservative nchini Uingereza kinadai kuanzishwa kwa uchunguzi rasmi kuhusu uamuzi wa marekani na Uingereza kuhusika katika vita vya Iraq mwaka 2003.