1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD:Milipuko wakati mahujaji waandamana

7 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCLO

Bomu moja limelipuka na kujeruhi polisi saba waliokuwa wakishika doria kulinda mahujaji wa KiSunni katika eneo la Wasunni wengi kusini mwa Baghdad.Kulingana na afisa mmoja wa usalama yapata polisi 15 na wakazi 10 wamejeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea wakati mahujaji hao walipoandamana mjini Saydiya wakibeba mabango na Quran.Msafara huo ulielekea mjini Karbala kwa tamasha la kidini.

Wakati huohuo mahujaji wa Kishia walifanya mashambulizi kufuatia mlipuko wa awali na kufikisha idadi ya vifo hadi 117.

Yapata walipuaji wa kujitolea muhanga wawili walijilipua pale kundi la Washia waliokuwa wakiandamana mjini Hilla kuelekea mji mtukufu wa Karbala kwa tamasha la kidini la Arbaeen.

Kulingana na Dr Saad al Shemari wa Hospitali ya Hilla aliyezungumza na Shirika la AFP la habari watu 173 zaidi wamejeruhiwa na idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.

Kulingana na Shirwan al Waili Waziri wa Usalama wa Kitaifa makundi matatu ya polisi wa usalama yamepelekwa mjini Karbala kuimarisha usalama.

Mwezi jana,Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki na wenza wake wa Marekani walizindua rasmi operesheni ya Fardh al Qanoon inazimia kudumisha sheria ili kuweza kusimamia mji wa Baghdad na kupoza ghasia kati ya makundi ya Washia na Wasunni.

Wakati huohuo Iran inatangaza kuwa itahudhuria kikao cha usalama mjini Baghdad kitakachowahusisha maafisa wa serikali ya Marekani.Mkutano huo unalenga kutoa nafasi ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani jambo ambalo ni nadra sana.Mjumbe maalum wa Marekani katika mkutano huo Zalmay Khalilzad anashikilia kuwa Marekani haina mpango wa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na nchi ya Iran japo iko tayari kuzungumzia suala la utumiaji wa silaha za Iran dhidi ya majeshi ya Marekani.