1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Waziri wa Ulinzi wa Marekani ziarani Iraq.

16 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBrQ

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates amewasili mjini Baghdad kwa ziara ya ghafla saa chache baada ya ndege ya kijeshi ya Marekani kuanguka.

Majeshi ya Marekani hayajatoa taarifa zaidi kuhusu ndege hiyo, lakini yamesema ndege hiyo ilikuwa na rubani peke yake na ilikuwa ikisaidia harakati za kijeshi za nchi kavu.

Waziri Robert Gates amesema Marekani haijaridhishwa na utendaji kazi wa serikali ya Waziri Mkuu Nouri al-Maliki.

Serikali hiyo imekuwa ikizozania mswada unaopendekeza jamii ya waislamu wachache wa madhehebu ya Sunni ipewe majukumu zaidi kwenye serikali na pia inufaike zaidi na mapato yanayotokana na mafuta ya petroli.

Robert Gates ameitembelea Iraq wakati huu muda mfupi baada ya shambulio la bomu la siku ya Jumatano kwenye msikiti wa madhehebu ya Shia katika mji wa Samarra.