BAGHDAD : Saddam kunyongwa katika kipindi cha siku 30 | Habari za Ulimwengu | DW | 27.12.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

BAGHDAD : Saddam kunyongwa katika kipindi cha siku 30

Mahkama ya Rufaa nchini Iraq imethibitisha hukumu ya adhabu ya kifo kwa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Saddam Hussein na kusema kwamba anapaswa kunyongwa katika kipindi kisichozidi siku 30.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Baghdad Hakimu Arif Shaheen amesema hukumu hiyo ni ya mwisho na inaibana kisheria serikali ya Iraq ambayo hivi sasa ina muda wa mwezi mmoja kumtia kitanzi Saddam na washtakiwa wenzake wawili.

Amesema utekelezaji wa hukumu hiyo hauwezi kupindukia siku 30 na inaweza kutekelezwa wakati wowote ule kuanzia leo hii.

Makundi ya Kutetea Haki za Binaadamu yamelaani kesi ya Saddam kuwa ilikuwa na dosari kubwa sana na wameitaka serikali kutoitekeleza hukumu hiyo.

Maafisa wa serikali ya Waziri Mkuu Nuri al- Maliki huko nyuma wamesema hawatosita kutekeleza hukumu hiyo na kwamba Saddam na washtakiwa wenzake wawili watanyongwa katika kipindi cha siku chache kufuatia uamuzi huo.

Wakili mkuu mtetezi wa Saddam Khalil al- Dulaimi amesema hukumu hiyo itazidi kuchochea mfarakano wa kimadhehebu nchini Iraq na ameita kuwa ya wenda wazimu na sio halali.

Saddam na washtakiwa wenzake sita walipatikana na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu kuhusiana na mauaji ya Washia 148 wa kijiji cha Dujail baada ya dikteta huyo kuepuka jaribio la kuuwawa hapo mwaka 1982.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com