Baba Mtakatifu Benedikt XVI ziarani Uturuki | Masuala ya Jamii | DW | 28.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Baba Mtakatifu Benedikt XVI ziarani Uturuki

Papa Benedikt XVI leo amewasili Ankara kwa ziara ya siku nne nchini Uturuki.Alipotoka kwenye ndege yake,alikaribishwa na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan binafsi na gwaride la heshima.

Waziri mkuu Erdogan ambae hadi hiyo jana haikujulikana kama ataonana na Papa Benedikt, alimkaribisha kwa ukunjufu Kiongozi wa Kanisa la Kikatoliki duniani kabla ya kuelekea Riga nchini Latvia kuhudhuria mkutano wa kilele wa shirika la kujihami la magharibi NATO.Erdogan baada ya kuzungumza na Papa Benedikt alisema ziara ya Benedikt ina umuhimu na inafanywa wakati wa muwafaka kwani ni muhimu kuzuia mapambano ya kitamaduni.Kwa mujibu wa Erdogan,Papa ameunga mkono juhudi ya Uturuki ya kutaka kuwa mwanachama katika Umoja wa Ulaya.Itakumbukwa kuwa mwaka jana,kabla ya kuchaguliwa kuwa Papa,Benedikt alisema,dini ya Kiislamu ya Uturuki humaanisha nchi hiyo haistahili kuwemo katika Umoja wa Ulaya.

Kwa hivyo Papa Benedikt amekwenda Uturuki akibeba mizigo miwili:upinzani wake maarufu kuhusu uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya na hotuba yake ya mwezi Septemba,ambayo Waislamu wengi wamesema imeutusi Uislamu.Papa alisema kuwa matamshi yake yameeleweka visivyo lakini hakuomba msamaha.

Ziara hii ya Papa nchini Uturuki,ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika nchi yenye Waislamu wengi, inafanywa chini ya ulinzi mkubwa.Hali ya usalama imeimarishwa na vikosi maalum vya ulinzi viliwekwa kwenye paa la jengo alikowasilia na uwanja wa ndege pia ulilindwa na wanajeshi.Kiasi ya askari polisi 3,000 wametawanywa pia katika mji mkuu Ankara kuzuia maandamano ya upinzani.

Juu ya hivyo,zaidi ya wazalendo 100 wa Kiislamu walikutana kati kati ya Ankara kuipinga ziara ya Benedikt.Wakati huo huo kama watumishi 50 wa serikalini pia walikusanyika kwa amani,mbele ya wizara ya masuala ya kidini ambako baadae Baba Mtakatifu alitarajiwa kukutana na kiongozi wa ngazi ya juu kuhusu mambo ya kidini nchini Uturuki.Siku ya Jumapili,kama Waturuki 25,000 waliandamana Istanbul kuipinga ziara ya Papa. Ingawa Waturuki wengi ni Waislamu,serikali yao ni ya kilimwengu.

Hii leo,baada ya kuonana na waziri mkuu Erdogan,Papa alikwenda kwenye kaburi la muasisi wa Jamhuri ya Uturuki ya kisasa,Mustafa Kemal Ataturk,ambako aliweka shada la muawa na akasoma sala fupi.

Papa Benedikt amesema,lengo la ziara yake ni kuendeleza uhusiano pamoja na Waislamu na pia Wakristo wa Kiorthodox.Katika kitendo cha upatanishi kwa wenyeji wake wa Kiislamu,Benedikt atatembelea msikiti maarufu wa mjini Istanbul. Lakini lengo kuu la ziara hii ya siku nne ni majadiliano kuhusu umoja wa Ukristo pamoja na Bartholomew-kiongozi mkuu wa Wakristo milioni 250 wa Kiorthodox alie na makao yake mjini Istanbul.