1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba mtakatifu ataka dunia iache vita

25 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCg9

Baba mtakatifu Benedicto wa tano ametaka kupatikana kwa suluhisho la mizozo iliyoigubika dunia, haswa mashariki ya kati na afrika.

Akizungumza katika ibada ya Krismas, Baba mtakatifu amesema pamoja na maendeleo yaliyopatikana duniani, lakini bado dunia inahitaji wokovu.

Amesema kizazi cha sasa kinahitaji wokovu kutokana na tishio la mmomonyoko wa siri wa maadili ya kijamii.

Baba mtakatifu alitoa ujumbe wake huo wa sikukuu ya Krismas kwenye misa iliyofanyika katika kanisa la mtakatifu Peter huko Vatican hii leo.

Mapema katika misa ya mkesha wa krismas jana usiku, baba mtakatifu Benedicto wa tano alitoa wito kwa dunia kuwasaidia watoto wanaokabiliwa na umasikini pamoja na wale waliajiriwa kama askari.

Papa Benedicto pia amepiga vita mambo maovu ambayo amesema kuwa yamekuwa yakitawala katika sikukuu ya krismas.

Huko Bethlehem ambako ndiko alikozaliwa yesu kristo zaidi ya miaka 200o iliyopita,rais wa mamlaka ya wapalestina Mahamoud Abbas alihudhuria mkesha wa misa ya krismas.

Padri Michel Sabbah aliyeendesha ibada hiyo alimbariki Mahamoud Abbas, na kutoa wito wa kumalizika kwa uhasama na umwagaji damu kati ya waisrael na wapalestina.

Sikuu ya Krismas inasherehekewa duniani kote ikiwa ni maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Mkurugenzi mkuu na wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio Deutche Welle wanawatakia krismas njema.