Assad aukataa ukanda maalumu | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Assad aukataa ukanda maalumu

Rais Bashar al Assad wa Syria amelikataa pendekezo la kutengwa ukanda maalumu wa huduma za kibinaadamu kwa wakimbizi ndani ya nchi hiyo akiliita kuwa ni la ajabu.

default

Portät Bashar al-Assad

Assad amekataa mpango huo kabla ya kuanza kwa mkutano wa dharura wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unaolenga kujadili kuporomoka kwa huduma za kibinaadamu nchini Syria.

Bashar al-Assad, Rais wa Syria

Bashar al-Assad, Rais wa Syria

Assad amekataa wazo hilo kwa sababu mbili, ya kwanza akisema kuwa mazungumzo ya mpango huo hayako mezani hadi sasa na ya pili akisema ni wazo lisilo halisi lililoibuliwa na maadui wa Syria.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Addounia kinachoegemea upande wa serikali yake Assad amesema: "Naamini kuzungumzia ukanda maalum wa wakimbizi si jambo halisi hata kwa nchi ambazo zina uaduia na syria. Licha ya makosa mengi yanayofanyika sasa, bado kuna mahusiano mazuri baina ya sera za mataifa hayo na imani za watu hawa".

Ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza hadharani tangu kufanyika kwa mauwaji ya washirka wa karibu kwenye serikali yake, Rais Assad amesema pia vikosi vyake vitaushinda mzozo unaoendelea nchini humo.

Assad ambaye amekumbwa na wimbi la kukimbiwa na viongozi wa ngazi za juu kwenye utawala wake, ameielezea hali hiyo kuwa ni kuisafisha nchi. Amesema kuwa serikali yake ilikuwa inafahamu kabla mipango yote ya viongozi hao walioasi.

Mkutano wa baraza la usalama

Mkutano wa leo wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mwanachama wa baraza la usalama la umoja wa mataifa unaweza kuathiriwa na kutokuwepo kwa viongozi wa ngazi za juu wa Marekani, China na Urusi na pengine usitoke na jambo la msingi katika kuutatua mzozo huo.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Ufaransa ambayo ndiyo rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Agosti, ina matumaini kuwa chombo hicho kitaungana kupata ufumbuzi. Uturuki, Lebanon na Jordani wanashiriki pia kwenye mazungumzo hayo.

Wachambuzi wanasema kuwa kando na kutangaza juhudi za kuipa msaada Syria mkutano huo hautatoka na jambo jingine la maana na wala hakutakuwa na hatua zozote mpya dhidi ya nchi hiyo.

Matumaini ya Uturuki

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmed Davutoglu

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmed Davutoglu

Uturuki ndiyo iliyotoa wazo hilo la kutengwa kwa maeneo ili kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na hatimaye kupunguza wimbi linaloingia nchi jirani. Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmed Davutoglu, amesema kuwa ni lazima hali hiyo ipatiwe ufumbuzi.

"Kulingana na sera za Uturuki, tumeongeza idadi ya kambi za wakimbizi. Tumeanzisha makambi mapya lakini hata tujenge vipi kambi hizo kama mashambulizi ya angani yanaendelea, sera ya kuwaangamiza watu kutokea mbali kama Bosnia itasababisha watu zaidi kuendelea kukimbia na kutafuta hifadhi Uturuki", alisema Davutoglu.

Aidha, Davutoglu anataraji Umoja wa Mataifa utaingilia kati na kuwalinda raia nchini humo na ikiwezekana kuwajengea mahema ndani ya ardhi yao.

Mwandishi: Stumai George/AFP/Reuters

Mhariri:Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com