Arsenal yajaribu mitambo yake kwa mafanikio
7 Agosti 2017Mjini London wachezaji wapya waliosajiliwa na Arsenal London mabingwa wa kombe la FA nchini Uingereza Alexandre Lacazette na Sead Kolasinac waling'ara katika pambano la kuashiria kufunguliwa msimu wa ligi ya England , kombe la ngao ya hisani , Community Shield jana Jumapili. Lakini kuchukulia ushindi huo wa Arsenal kuwa mwelekeo wa ligi hiyo ni makosa, hata hivyo kuna ishara chanya kwa Arsenal kufuatia ushindi wa mabao 4-1 katika mikwaju ya penalti dhidi ya mahasimu wao mjini London Chelsea.
Kocha wa Arsenal London Arsene Wenger anaamini nguvu za mashindano katika ligi ya England Premier League , ina maana timu yake haiwezi kuanza vibaya iwapo watataka kupambana kunyakua ubingwa huo. Arsenal ilipoteza michezo yake mitatu ya mwanzo , mwanzoni mwa ligi hiyo msimu uliopita, baada ya kupoteza mchezo wa nyumbani dhidi ya Liverpool kwa mabao 4-3 na kuweka msimamo wa ligi ambapo ilishindwa kufuzu kuingia katika timu za Champions League kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1997.
Kikosi cha Wenger kinajitupa uwanja kwa msimu mpya kupambana na Leicester City siku ya Ijumaa na amewataka wachezaji wake kutumia ushindi wa jana kuweza kuanza vizuri msimu ujao kwa ushindi.
Mwandishi: Sekione Kitojo/dpae,afpe,rtre,ape
Mhariri: Mohammed Khelef