1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria kumenyana na Senegal fainali ya Afcon 2019

Bruce Amani
15 Julai 2019

Pazia la mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon 2019 litafungwa mjini Cairo kwa kuandaliwa fainali ya kukata na shoka. Afrika Magharibi inakutana na Afrika Kaskazini

https://p.dw.com/p/3M6wE
Afrika Cup 2019 | Riyad Mahrez und Sadio Mane
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Schalit

Senegal watashuka dimbani na Algeria. Algeria ilitinga fainali baada ya Riyad Mahrez kufunga freekick safi sana katika dakika ya tano ya muda wa majeruhi na kupata ushindi wa 2 – 1 dhidi ya Nigeria. Senegal nao walifuzu baada ya ushindi wa 1 – 0 dhidi ya Tunisia katika muda wa ziada baada ya mechi kukamilika bila kufungana katika muda wa ziada.

Algeria wanawinda Kombe la Afrika kwa mara ya pili na lao la kwanza katika karibu miaka 30. Senegal wanawinda taji lao la kwanza la Afrika baada ya miaka 54 ya kujaribu.

Timu zote zilikutana katika hatua ya makundi, Kundi C ambapo Algeria ilipata ushindi wa 1 – 0.

Fainali hiyo itakuwa pia itakuwa na sura ya uhasama wa Premier League wakati Mahrez wa Manchester City (mabingwa wa ligi) atakutana na Sadio Mane wa Liverpool (makamu bingwa). Mechi zote za nusu fainali zilikuwa na vituko vya maamuzi yaliyochangiwa na mfumo wa VAR.

Algeria waliongoza kupigia bao la kujifunga Senegal katika kipindi cha kwanza la William Troost-Ekong. Nigeria ikapewa penalty kutokana na kuunawa mpira baada ya refarii wa Gambia Bakary Gassama kutizama VAR, ambaye awali hakuwa amepeana penalty. Nigeria wakasawazisha kupitia Odion Ighalo. Lakini Mahrez akafunga freekick na kuwazika Nigeria.

Afrika-Cup 2019 Halbfinale | Algerien - Nigeria
Algeria waliwafunga Nigeria 2 -1Picha: Getty Images/AFP/F. Senna

"Tayari tulikuwa na morale, nadhani, lakini mechi hii imetupa matumaini zaidi ya kucheza katika fainali. Yatakuwa mapambano mengine, mechi nyingine ngumu, lakini nadhani tuna uwezo wa kushinda. Tulicheza dhidi ya Senegal katika hatua ya makundi. Ni timu nzuri sana, na tutaona itakavyokuwa.

Kocha wa Algeria Djamel Belmadi amesema timu yake haikuhisi kama wapinzani wao walistahili penalt waliyopewa na kuwa walitaka kumaliza mechi kabla ya muda wa ziada kuanzishwa.

Tulihisi kuwa haikuwa haki laini tunapaswa kuona video tena lakini hicho ndicho tulichohisi na hatukutaka kuingia muda wa ziada. Hata kama tungelazimika kucheza muda wa ziada tungefanya tuwezavyo lakini wachezaji walitaka kushinda mechi kabla na walitengeneza nafasi na kurejea mchezoni na kuamini hadi mwisho. Hilo litatusaidia katika siku za usoni. Sio mbali sana.

Kocha wa Nigeria Gernot Rohr hakuwa na sababu yoyote ya kulalamika na akakiri kuwa kandanda ni kandanda.

"Freekick maridadi kabisa kutoka kwa mchezaji nyota ndio iliyoleta tofauti. Mara ya mwisho tulishinda katika dakika ya mwisho dhidi ya Afrika Kusini. Leo tumepoteza na hilo ndio kandanda.

Afrika-Cup 2019 Halbfinale | Senegal - Tunesien
Senegal waliwashinda Tunisia 1 - 0 kupitia bao la kujifungaPicha: Reuters/S. Salem

Senegal na Tunisia zilikosa penalty katika muda wa kawaida. Tunisia walipewa penalty nyingine katika dakika za mwisho za muda wa ziada lakini Refarii Muethiopia Bamlak Tessema Weesa akaangalia VAR na kuubatilisha uamuzi huo.

Kocha wa Senega Aliou Cisse alisema mechi hiyo itabaki katika kumbukumbu ya kandanda la Afrika kutokana na vituko vilivyoshuhudiwa.

"tunajivunia kwa sababu ni miaka 17 tangu tufike hatua hii, tangu kizazi cha 2002, na ni kutokana na kazi ngumu na uvumilivu. Mimi ni miongoni mwa wanaojiweka mchezoni kutokea kwenye benchi, napenda kuwa na vijana wangu, kuhisi uchungu wanaopitia na kuwapa motisha. Kazi hii imeendelea kwa zaidi ya miaka mitano

Naye kocha wa Tunisia Alain Giresse alisema timu yake ilipambana vilivyo dhidi ya Senegal lakini ikajutia kukosa kufunga penalty

Wakati tulipoondolewa, ni kitu cha kwanza kilichoumiza. Katika aina hizi za mechi kitu muhimu ni kufuzu, kucheza hadi mwisho wa mashindano. Haikuwa hivyo kwetu lakini tunaweza kusema tulicheza kiwango sawa na timu ya Senegal na viwango vya nusu fainali. Lakini ndio hivyo katika kandanda, tulikuwa na nafasi lakini bahati mbaya hatukuzitumia, labda penalty ambayo hatukufunga ingebadilisha matokeo lakini tumeondolewa usiku huu.