1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya amani huenda ikarejea Cote d'Ivoire

26 Oktoba 2015

Rais wa sasa wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara anapewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Jumapili ukiwa ni uchaguzi wa kwanza kufanyika baada ya ule uliofanyika mwaka 2010.

https://p.dw.com/p/1GuCs
Rais wa sasa wa Ivory Coast Alassane Ouattara
Rais wa sasa wa Ivory Coast Alassane OuattaraPicha: AFP/Getty Images/I. Sanogo

Vituo vya upigaji kura vilifungwa saa tisa alasiri baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura na matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa ndani ya siku tano.

Ivory Coast ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa zao la kakao duniani ilihitaji kuwa na uchaguzi wenye amani ambao ungesaidia kurejesha hadhi iliyokuwa nayo ya kiuchumi hapo kabla barani Afrika.

Zaidi ya watu milioni sita walipiga kura katika uchaguzi huo.

Kiasi cha wanajeshi 34,000 miongoni mwao 6,000 wakiwa wa umoja wa mataifa walikuwa wakifanya doria wakati wa zoezi la upigaji kura la Jumapili.

Kufikia mchana wa jumapili ni asilimia 45 tu ya wapiga kura waliokuwa wamejitokeza ukilinganisha na asilimia 80 ya walioshiriki katika uchaguzi wa mwaka 2010.

Muda wa upigaji kura ulirefushwa ingawa bado kuna baadhi ya watu waliojiandikisha ambao hawakuweza kupiga kura.

Ouattara kushinda katika mzunguko wa kwanza

Ouattara, mchumi maarufu na ambaye amewahi kushika moja ya nafasi za juu katika shirika la kimataifa la fedha duniani ( I.M.F ) anatarajiwa kushinda kwa kishindo katika mzunguko wa kwanza na kuzima uwezekano wa kurudiwa kwa kura za urais katika uchaguzi huo.

Ouattara mwenye umri wa miaka 73 amepania kufufua uchumi na kurejesha hali ya utulivu katika taifa hilo ambalo ni koloni la zamani la Ufaransa.

Hali ya utulivu ilitoweka siku chache baadaya upigaji kura wa mwaka 2010 kufuatia Rais wa wakati huo Gbabo kukataa kukubali kushindwa baada ya Ouattara kutangazwa kuwa mshindi.

Ouattara hatimaye aliapishwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 2011 na Gbabo aliondolowa kwa nguvu madarakani na majeshi yaliyokuwa yakimuunga mkono Ouattara kwa msaada wa serikali ya Ufaransa.

Gbabo kwa sasa anakabiliwa na kesi katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa iliyoko the Heague nchini Uholanzi.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/APE

Mhariri : Daniel Gakuba