1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Bashir kujiondoa mazungumzo ya Doha

Admin.WagnerD30 Desemba 2010

Rais wa Sudan Omar-Al Bashir, amesema serikali yake itajiondoa katika mazungumzo ya amani na vyama vya waasi vya Darfur, yanayofanyika mjini Doha, ikiwa hakutafikiwa makubaliano yoyote leo, Alhamis, Disemba 30, 2010

https://p.dw.com/p/zrUR
Rais Omar Hassan Al-Bashir wa Sudan
Rais Omar Hassan Al-Bashir wa SudanPicha: AP Photo

Omar Hassan Al-Bashir, amewaambia wafuasi wake katika mji wa Nyala wa mkoa wa magharibi mwa Sudan wa Darfur, kwamba atamshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa makubaliano na muungano wa vyama vya waasi yatafikiwa leo Alhamisi.

Akasema kuwa la sivyo, basi serikali yake itajiondoa katika mazungumzo hayo yanayofanyika katika mji mkuu wa Qatar- Doha.

" Tutaendesha vita dhidi ya wale walioamua kutumia silaha, lakini tutaketi na kuzungumza na wale wanaotaka maendendeleo" aliendelea kusema Al-Bashir, huku akishangiliwa na mamia kwa maelfu ya wafuasi wake.

Chama kikubwa cha waasi wa Darfur cha JEM hakikuchelewa kujibu madai hayo ya Rais Al-Bashir. Msemaji wa chama hicho Ahmed Hussein Adam Said, ameliambia shirika la habari AFP, kwamba matamshi ya Bwana Al-Bashir, ni kama tangazo la vita.

"Tunalani matamshi ya Al-Bashir. Yanalenga kukwamisha juhudi za jamii ya kimataifa na wapatanishi, za kufikia suluhisho la mzozo wa uliopo kwa njia za kisiasa"; alisisitiza msemaji huyo wa chama cha JEM.

Mjumbe wa Jumuiya ya Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika katika mazungumzo baina ya serikali ya Sudan na vyama vya waasi wa Darfur huko mjini Doha, Bwana Djibril Bassole, amesema kwamba atajaribu kuzishawishi pande mbili kuendelea na mazungumzo, hata kama makubaliano hayatafikiwa leo au kesho. Amesema kwamba yeye ni miongoni mwa wawakilishi wa jamii ya kimataifa wanaofanya kila wawezalo ili yafikiwe makubaliano ya amani yanayoridhisha kila upande, lakini ni vigumu kuendesha mazungumzo na watu ambao wameishika saa mkononi; akimaanisha hali ya kuwekwa tarehe ya mwisho ya mazungumzo.

Wanajeshi watoto katika jeshi la waasi wa Sudan
Wanajeshi watoto katika jeshi la waasi wa SudanPicha: AP

Miezi mitatu iliyopita, serikali ya Sudan ilikuwa tayari imeshasema kwamba ikiwa hakutapatikana makubaliano ifikapo tarehe thelathini na moja ya mwezi Desemba, basi itajiondoa mara moja katika mazungumzo ya Doha.

Watu zaidi ya laki tatu wameuwawa kutokana na vita baina ya majeshi ya serikali ya Karthoum na makundi ya waasi wa eneo la maghribi mwa Sudan la Darfur. Zaidi ya raia miliyoni mbili na laki saba wamelazimika kuyahama makaazi yao kutokana na vita hivyo. Rais Omar Al-Bashir anakabiliwa na waraka wa kumukamata, uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya vitendo vya jinai; akituhumiwa kuunga mkono vitendo vya kikatili na mauwaji ya kivita, vilivyoendeshwa na makundi ya wanamgambo wanaomtii.

Mwandishi: Jean-Francois Gisimba / AFP

Mhariri: Josephat Charo