1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Ahly yavunjiwa rekodi ya miezi 30 ya kutoshindwa nyumbani

8 Januari 2007

Mabingwa wa Afrika Al Ahly ya Misri wakomewa mabao 3:0 na Ismailia.Stuttgart ina miadi na Berlin katika Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani na Kombe la klabu bingwa za Afrika Mashariki laanza mjini Kigali.

https://p.dw.com/p/CHcp

Katika kura iliopigwa jana, VFB Stuttgart imepigiwa kura ya kuonana na Hertha Berlin katika mchuano wa robo-finali wa Kombe la shirikisho.Stuttgart imeshatoroka mara 3 na kombe hili-mara ya mwisho ikiwa 1997.Berlin bado haikulitwaa licha ya kwamba finali zake huchezewa nyumbani mwao-katika Berlin Olympic Stadium.

Katika mpambano mwengine wa robo-finali-Nuremberg ina miadi na Hannover 96 wakati Wolfsburg wataonana na Alemania Aaachen-timu iliopanda daraja ya kwanza msimu huu tu na ilioipiga kumbo mabingwa watetezi-Bayern Munich.Mapambano mengine yanajumuisha Offenbach ya daraja ya pili na Eintracht Frankfurt ya daraja ya kwanza.

Robo-finali hizo zimepangwa Februari 27 na 28.

Oliver Kahn,aliewahi kuchaguliwa mara 3 “kipa bora wa dunia”,aliarifu jana kwamba huu yamkini ukawa msimu wake wa mwisho na mwakani atastaafu utakapomalizika mkataba wake na Bayern Munich.

Mwaka ujao,Oliver Kahn atafikia umri wa miaka 39 na anasema wakati umewadia nae kutundika glovu zake ukutani.Kahn alichangia mno kuisadia Bayern Munich kutwaa kombe la Ulaya la klabu bingwa-champions League pale alipookoa mikwaju 3 ya penalty wakati wa finali na Valencia.

Tukisalia bado katika viwanja vya dimba la Ujerumani, Uli Hoeness-meneja wa Bayern Munich-mabingwa wa Ujerumani, amesema mchezaji wa giungo wa Uingereza Owen Hargreaves,anaeichezea Bayern Munich hatauzwa kwa Manchester United katika soko la sasa la majira ya baridi la kuuza wachezaji,labda lakini, mwishoni mwa msimu huu.Hargreaves,ambae hakucheza dimba tangu kuumia Septemba 17,mwaka uliopita amekuwa akiiomba sana klabu yake ya Ujerumani kumuachia kujiunga na Manchester.Hii inafuatia hodi hodi ilizopiga Manchester united baada ya Kombe la dunia nchini Ujerumani mwaka jana.

Arsenal kesho impania kuipa changamoto kali FC Liverpool katika kinyan’ganyiro cha robo-finali cha Kombe la FA:Liverpool hawakushindwa bado nyumbani katika Premier League, tangu Oktoba mwaka jana .

Na baada ya kulazwa katika champions league na Benefica Lisbon, Liverpool haitaiachia Arsenal kuondoka na ushindi.Liverpool,lakini itapaswa kumchunga mcheki Tomas Rosicky alietia mabao 2 jumamosi pamoja na nahodha Thierry Henry,alleanza kuona tena mango.

Huko Spain, FC Barcelona-mabingwa na mahasimu wao Real Madrid, walirudi uwanjani baada ya likizo ya mwaka mpya lakini, bila kufua dafu.Barcelona iliondokea suluhu bao 1:1 na Getafe, wakati Real walikiona kwa mara ya pili “kile kilichomtoa kanga manyoya” kwa kuzabwa mabao 2:0 na Deportivo la coruna.

Huko Ufaransa Paris st.Germain, ilitamba mwanzoni mwa kinyan’ganyiro chake cha kutetea taji lao la Kombe la Ufaransa.Paris St.Germain iliionea timu ya daraja ya 3 Nimes mabao 3:0.

Na huko Ureno,mabingwa wa kombe la shirikisho Porto walitimuliwa nje ya kombe hilo jana baada ya kulazwa nyumbani bao 1:0 na timu ya daraja ya pili ya Atletico katika duru ya 4 ya kombe hilo.

Huko Ruanda, kinyan’ganyiro cha kombe la klabu bingwa za Africa mashariki na kati-Kagame Cup-kimeanza mwishoni mwa wiki huku mabingwa watetezi-Polisi ya Uganda wakijiwinda kurudi na Kombe Kampala.Young Africans ya Tanzania,imeshaipelekea salamu Polisi,kwamba –mramba asali harambi mara 2:

Tukibakia katika kabumbu, si chini ya wachezaji 12 wa klabu mashuhuri ya ya Nigeria-Nasarawa united walifikishwa hospitali kwa majaraha mbali mbali baada ya wezi waliokuwa na silaha kuvamia kambi yao ya mazowezi mapema jana.

Kocha wao Zakary Baraje akithibitisha mkasa huo amesema sehemu kubwa ya wachezaji walioumia ni wa daraja ya kwanza katika timu hiyo.Chama cha mpira cha Nigeria, kikaahirisha mechi yao ya kwanza numbani dhidi ya Dolphins iliokua ichezwe jana.

Nao mabingwa wa Afrika, Al Ahli ya Misri wameonja shubiri yao ya kwanza nyumbani:Rekodi yao ya kutolazwa nyumbani ya miezi 30 ilivunjwa jana na Ismailia baada ya kukomewa mabao 3:0.Hilo likawa pigo la kwanza kwa Al Ahly-mabingwa wa Afrika, tangu walipokumtwa na Arab Contractors Julai, 2004.

Nae kocha wa klabu ya Aviacao ya Angola, mreno Bernardino Pedroto alieiacha mkono klabu yake ya Angola ya AS Aviacao mapema wiki iliopita,sasa ni kocha mpya wa mahasimu wa Aviacao-Petro Atletico.

Pedroto aliiaga Aviacao kwa kuwa iliamua kuwauza wachezaji wake mashuhuri kutokana na shida za fedha.

Na katika Ligi ya Afrika Kusini,Silver Stars wako kileleni baada ya kuwalaza Golden Arrows mabao 3:1.Wits University inasimama nafasi ya pili huko Kaizer Chief ikinyatia nafasi ya 3 licha ya kuzabwa mabao 2:0 jumamosi na SuperSport United.