1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya ndege Libya

Kabogo Grace Patricla12 Mei 2010

Watu 103 wafa katika ajali ya ndege iliyotokea Libya, huku manusura pekee akiwa mtoto wa miaka 9 raia wa Uholanzi.

https://p.dw.com/p/NMME
Timu ya waokozi wakiwa mjini Tripoli, Libya katika eneo ilipotokea ajali ya ndege ya shirika la ndege la nchi hiyo, Afriqiyah.Picha: AP

Mtu mmoja tu aliyenusurika katika ajali ya ndege ya Shirika la nchi hiyo la Afriqiyah. Taarifa zinasema aliyenusurika katika ajali hiyo iliyowauawa abiria na wafanyakazi 103 wa ndege hiyo ni mtoto mmoja wa kiume raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 9. Wizara ya Nje ya Uholanzi pia imesema miongoni mwa waliouawa ni raia 61 wa nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Uholanzi, Ozlem Canel ameliambia shirika la habari la AFP mjini The Hague kuwa mtoto huyo raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka tisa anatibiwa kutokana na majeraha aliyoyapata katika ajali hiyo. Ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Afrika Kusini kwenda Libya, ilianguka mapema leo wakati ikijaribu kutua katika uwanja wa ndege wa Tripoli na kuwaua watu 103 waliokuwemo ndani, huku mtoto huyo akiwa manusura pekee.

Abiria 61 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo chapa A330-200 ambayo imekuwa ikifanya safari zake tangu mwezi Septemba mwaka uliopita, ni raia kutoka Uholanzi. Waziri Mkuu wa Uholanzi, Jan Peter Balkenende amesema ndege hiyo ilikuwa na abiria wengi wa Uholanzi. Nao maafisa wa Libya wamesema abiria wengine 22 walikuwa raia wa Libya, lakini hawajatoa taarifa zaidi kuhusu uraia wa abiria wengine. Akizungumza na waandishi habari kwenye uwanja wa ndege wa Tripoli, Waziri wa Usafiri wa Libya, Mohamed Zidan alisema kuwa abiria wote ndani ya ndege hiyo wameuawa isipokuwa mtoto huyo wa kiume.

Maafisa wa Libya na viongozi wa shirika hilo la ndege la Afriqiyah wamesema ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 93 na wafanyakazi wake 11. Hata hivyo, Waziri Zidan amesema mtoto huyo yuko katika hali nzuri. Viongozi wa shirika hilo la ndege wamesema kuwa ajali hiyo ni ya kwanza kuwahi kutokea katika historia ya shirika hilo tangu lianzishwe mwaka 2001. Shirika hilo limeelezea masikitiko yake kutokana na ajali hiyo na limetoa salamu za pole kwa familia na marafiki wa watu waliouawa katika ajali hiyo.

Mkuu wa idara ya masuala ya kisheria wa shirika hilo la ndege, Saleh Ali Saleh ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kuwa kisanduku cha kunasa sauti cha ndege hiyo kimepatikana kutoka eneo ilipotokea ajali hiyo. Bwana Saleh Ali amesema kuwa uchunguzi unaendelea.

Picha za shirika la habari la Reuters kutoka katika eneo la ajali zimeonyesha vipande vya ndege hiyo pamoja na mizigo ya abiria, huku mkia wa ndege hiyo uliopambwa kwa nembo ya shirika hilo yenye rangi nyekundu, kijani na manjano ukionekana kuegemea upande mmoja. Mwandishi habari wa Reuters aliyekuweko katika uwanja wa ndege wa Tripoli amesema magari ya wagonjwa yalikuwa yakipeleka miili ya abiria hao katika vyumba vya kuhifadhia maiti kwenye hospitali za mjini Tripoli.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman