1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

28 Agosti 2015

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya wakimbizi kutoka Eritrea, kuapishwa kwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na juu ya mtanziko wa lugha unaowakabili watoto wa barani Afrika

https://p.dw.com/p/1GNZO
Burundi Vereidigung Präsident Nkurunziza
Picha: Reuters/E. Ngendakumana

Gazeti la "Süddeutsche" wiki hii limeandika juu ya wakimbizi wa Eritrea.Gazeti hilo linasema ni kutokana na sera ya serikali ya Eritrea kwamba vijana wanaamua kuikimbia nchi yao.

Gazeti hilo linaeleza kwamba idadi kubwa kabisa ya wakimbizi wanaojaa katika mashua zinazojaribu kuvuka bahari ya Mediterania ili kuenda Ulaya ni ya watu wanaotoka Eritrea. Watu hadi 5000 wanakimbia Eritrea karibu kila mwezi .

Gazeti la "Süddeutsche" linasema ni vigumu kujua kwa nini watu wengi wanaikimbia nchi yao. Ni vigumu kwa vyombo vya habari lakini pia kwa Umoja wa Mataifa. Gazeti hilo linafahamisha kwamba tume ya haki za binadamu ya Umoja huo ilichapisha ripoti juu ya hali ya nchini Eritrea,inayodai kwamba serikali ya Eritrea inawakandamiza wananchi wake na inasababisha hofu miongoni mwa wananchi. Hata hivyo gazeti hilo linatilia maanani kwamba ripoti hiyo ilitokana na majibu yaliyotolewa na Watu wa Eritrea walioko nje ya nchi.

Gazeti la "Süddeutsche" linakumbusha kwamba alipoingia madarakani Rais Isaias Afwerk aliashiria matumaini kwa watu wake nchini Eritrea.Lakini baadae alianza kuutumia mgogoro na Ethiopia, kuwalazimisha vijana wa nchi yake kulitumikia jeshi.

Nkurunziza aapishwa

Gazeti la "die tageszeitung" linaarifu juu ya kuapishwa kwa Rais Pierre Nkurunziza nchini Burundi. Gazeti hilo linasema hafla ya kuapishwa Rais huyo ilikuwa ya kushtukiza. Gazeti hilo linafahamisha kwamba hapo awali tarehe ya kuapishwa Rais hiyo ilipangwa vingine. Lakini gazeti la "dia tageszeitung" linatilia maanani kwamba kuapishwa kwa bwana Nkurunziza maana yake ni kuanza kuutumikia muhula wa tatu wa urais, baada ya kushinda uchaguzi kwa kupata asilimia 69 ya kura mnamo mwezi uliopita.

Gazeti la "die tageszetung" limemnukulu Rais Nkurunziza akisema baada ya kuapishwa, kwamba kuapishwa kwake,ni uthibitisho kuwa hakuna binadamu anaeweza kuliambia jua liache kuangaza.

Lakini gazeti la "die tageszeitung" linaarifu kuwa vyama vya upinzani karibu vyote haviutambui urais wa Nkurunziza. Agathon Rwasa ndiye kiongozi pekee wa upinzani aliempongeza Rais Nkurunziza.

Gazeti la "Berliner" wiki hii linazungumzia juu ya mashindano ya riadha ya ubingwa wa dunia mjini Beijing. Gazeti hilo linawazungumzia wanariadha wawili wa Kenya waliogundulika kuwa wanatumia dawa za kuongeza nguvu

China Leichtathletik WM Joyce Zakary
Picha: Getty Images/A. Lyons

Gazeti hilo linasema ni wanariadha wawili tu wa Kenya waliofikwa na aibu hiyo lakini wameuwasha moto usioweza kuzimika . Gazeti la "Berliner" linasema, habari juu ya wanariadha hao walioanguka mtihani, zilitolewa wakati ambapo Kenya imekanusha madai kwamba wakimbiaji wake wanatumia madawa ya kuongeza nguvu.

Gazeti la "Berliner "limewanukuu wadau wa michezo nchini Kenya wakisema kwamba washindani barani Ulaya wanayaonea gele mafanikio ya Kenya.

Lugha nyingi zawatatiza watoto barani Afrika

Gazeti la "Süddeutsche" wiki hii pia linazungumzia juu ya kazi kubwa inayowapata watoto barani Afrika ya kuzungumza lugha zaidi ya tatu katika maisha yao ya kila siku. Gazeti hilo linatoa mfano wa mtoto Dotto Kitwenga mwenye umri wa miaka 18 kutoka Tanzania.

Gazeti hilo linasema mtoto huyo anaesoma kwenye shule ya upili anazumgumza kiswahili anapokuwa pamoja na ndugu na marafiki zake nyumbani.Lakini anapozungumza na wazazi wake anatumia lugha ya kisukuma, na shuleni masomo yanafundishwa katika lugha ya kiingereza. Gazeti la "Süddeutsche" limeandika katika makala yake kwamba Dotto, sawa na watoto wengine nchini Tanzania amezungukwa na lugha zaidi ya 120.

Hata hivyo gazeti hilo linaeleza kuwa Tanzania siyo inayoongoza kwa idadi ya lugha barani Afrika. Lugha karibu 280 zinazungumzwa nchini Camerun na karibu 520 zinazungumzwa nchini Nigeria.

Gazeti la "Süddeutsche" limewanukulu watafiti wanaofahamisha kuwa lugha zipatazo 2000 zinazungumzwa barani Afrika. Gazeti hilo linasema kutokana na utata huo, lugha zilizopelekwa na wakoloni barani Afrika bado zinatumika kwenye mabunge ya nchi kadhaa.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Mohammed Khelef