1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya12 Agosti 2012

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya ziara ya Waziri Hillary Clinton barani Afrika na juu ya ziara ya Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel magharibi mwa Afrika.

https://p.dw.com/p/15oFX
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel nchini Mali
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel nchini MaliPicha: picture-alliance/dpa

Magazeti ya Ujerumani pia yanauliza iwapo raslimali zinazogunduliwa barani Afrika ni neema au laana!

Gazeti la "Süddeutsche Zeitungen" limetoa maoni juu ya ziara ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton katika nchi kadhaa za Afrika. Na linasema "Mabadiliko makubwa yametokea barani Afrika-bara ambalo hadi miaka ya hivi karibuni tu lilikatiwa tamaa kabisa.

Gazeti hilo linahoji kuwa Marekani haiwezi kuyapuuza mabadiliko hayo ya maendeleo.Uchumi wa nchi nyingi za Afrika unastawi katika kiwango kisichokuwa na mithili kwingineko duniani.Na ustawi huo hautokani na malighafi tu. Linasema ni mapema mno kusema kuwa "Simba" wa Afrika atazifuata nyayo za "Chui" wa Asia, lakini hakuna anaeweza kuupuuza umuhimu wa kiuchumi na kisiasa wa bara la Afrika. Gazeti la "Süddeutsche Zeitung"linasema katika maoni yake kwamba ziara ya Waziri Clinton barani Afrika pia imelenga shabaha ya kutoa ishara kwa China na Brazil kwamba Marekani bado ni rafiki wa Afrika.

Ujerumani yatoa mwito wa kuleta suluhisho nchini Mali kwa njia ya mazungumzo.Hizo ni habari zilizochapishwa na gazeti la "Frankfurter Allgemeine" juu ya ziara ya waziri wa maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel magharibi mwa Afrika. Gazeti hilo linaarifu zaidi kwamba Waziri Niebel amefanya ziara nchini Mali na amekutana na viongozi wa serikali ya mpito wa nchi hiyo.Lakini kabla ya hapo waziri huyo alizitembelea Sierra Leone na Burkina Farso. Waziri Niebel ameahidi kuongeza msaada wa maendeleo kwa nchi hizo

Katika makala yake gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatilia maanani kwamba Ujerumani ilikuwa mshirika muhimu wa Mali katika masuala ya maendeleo kabla ya utawala halali wa nchi hiyo kuangushwa na wanajeshi mnamo mwezi wa machi.

Viongozi wa nchi za eneo la maziwa makuu walikutana mjini Kampala ili kuujadili mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokarasi ya Kongo. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "die tageszeitung" Gazeti hilo linasema licha ya mkutano wa viongozi kufanyika, vita vinaendelea mashariki mwa Kongo, na linaeleza kwamaba mkutano wa viongozi wa nchi za eneo la maziwa makuu ulipaswa kupitisha hatua muhimu juu ya vita vya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yaani kuunda kikosi ili kuzima uasi katika sehemu hiyo. Lakini badala yake viongozi hao waliumaliza mkutano wao kwa kukukabiliana kukutana tena katika wiki nne zijazo.
Gazeti la "die tageszeitung " limetathmini kushindwa kwa viongozi wa nchi za maziwa makuu kuunda kikosi haraka, kuwa ni kuendelea kwa mapigano mashariki kwa Kongo.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" linahoji kwamba nchini zenye utajiri wa malighafi, barani Afrika zimekaliwa vibaya katika maendeleo kuliko zile ambazo hazina mali ghafi nyingi. Na linauliza jee utajiri wa malighafi kama mafuta ni neema au balaa kwa nchi za Afrika.

Gazeti hilo linaeleza kuwa zipo sababu kadhaa.Linasema mtu angefikiri kwamba mapato yanayotokana na mauzo ya maliasilia yangeliekezwa katika maendeleo ya watu katika nchi hizo. Lakini balaa linatokea kutokana na sababu kadhaa. Sarafu za nchi hizo zinakuwa na thamani ya juu,jambo linalotatanisha mauzo nje, Pili ugeu geu wa bei za malighafi kwenye masoko ya dunia, unaathiri mipango ya maendeleo ya nchi husika, na vile vile nchi hizo haziekezi mapato yanayotokana na mauzo ya malighafi zao katika sekta za mendeleo.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" limezitaja baadhi ya nchi zenye utajiri wa malighafi, ikiwa pamoja na Ghana, Uganda, Msumbiji na Tanzania. Gazeti hilo pia linasema mikataba mibaya baina ya nchi hizo na makumpuni ya kimataifa inachangia katika kusababisha madhara katika maendeleo ya nchi hizo.


Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu