Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 06.07.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya ustawi imara wa uchumi barani Afrika na pia yanakumbusha juu ya historia ya Ujerumani katika bara hilo

Waherero waliotekwa na Wajerumani, Namibia 1904

Waherero waliotekwa na Wajerumani,Namibia 1904

.Katika makala yake gazeti la "Der Spiegel" linalizingatia tabaka la watu wa kati nchini Uganda na linaeleza kuwa wakati sehemu zingine za dunia zimekumbwa na migogoro ,uchumi wa nchi za Afrika, za kusini ya jangwa la Sahara unastawi mtindo mmoja. Gazeti la "Der Spiegel" linatilia maanani katika makala yake kwamba,bara la Afrika linastawi siyo kutokana na kuuza malighafi tu.

Gazeti la "Der Spiegel" linatoa mfano wa msanii wa mitindo ya mavazi kutoka Uganda,Sylvia Owori. Gazeti hilo linasema kuwa Sylvia Owori amepata mafanikio ya juu kabisa. Mama huyo anamiliki maduka ya nguo katika miji ya Kampala na Nairobi. Mitindo yake ya nguo inaonekana katika mitaa ya Paris na Rome kwa kupitia kwa mawakala wake. Gazeti la"Der Spiegel" linasema katika makala yake kuwa mafanikio ya Sylvia Owori yanawakilisha ustawi wa tabaka la kati barani Afrika .

Gazeti hilo linasema kutokana na ustawi wa uchumi tabaka la kati linainukia barani Afrika. Gazeti la " Der Spiegel"linatilia maanani kwamba, katika nchi 10 duniani, zinazostawi kiuchumi kwa nguvu,tano zipo barani Afrika.

Gazeti la "Die Presse" pia limeandika juu ya ustawi wa uchumi barani Afrika.Pia linatilia maanani kwamba miongoni mwa nchi 10 zinazostawi vizuri kiuchumi duniani,nusu yake zipo barani Afrika. Gazeti la "Die Presse" limeandika: "Mara tu mtu anaposikia juu ya Afrika, haraka sana akili yake inachora picha ya watoto wenye njaa, vita na rushwa."Lakini gazeti hilo linasema pia zipo habari nzuri juu ya Afrika. Uchumi unastawi na jamii zinabadilika . Tabaka la kati linainukia, lenye uwezo wa kutoa fedha na kununua bidhaa kama magari na kulipa ada za shule za watoto kwa njia ya simu.

Gazeti la "Financial Times Deutschland" nalo linazungumzia juu ya habari nzuri kutoka Angola. Gazeti hilo limearifu juu ya matumaini ya kupatikana mafuta zaidi nchini Angola.Hata hivyo gazeti hilo linasema kiasi kikubwa cha vitega uchumi kitahitajika kwa ajili ya mradi huo.

Gazeti la "die tageszeitung" linatupeleka Ghana ambako pametokea mvutano baina ya wafanyabiashara wa nje na serikali ya nchi hiyo. Gazeti hilo linaarifu kuwa Serikali ya Ghana haitaki mchezo! Tokea Jumanne biashara na vibanda vya raia wa nje vinafungwa. Vikosi maalumu vinaifanya kazi hiyo. Gazeti la "die tageszeitung" limeripoti kwamba serikali ya Ghana imepitisha sheria kwa wafanyabiashara kutoka nchi za nje ikiwa pamoja na Waafrika wanaotoka nchi zilizomo katika jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi Ecowas.

Sheria hiyo inawataka wafanyabiashara hao wafungue biashara zao kwenye sehemu zilizotengwa maalumu .Na kila mfanyabiashara wa nje afungue biashara thamani ya dola laki tatu na lazima awaajiri wananchi wa Ghana angalau kumi.

Gazeti la "die tageszeitung limemnukuu waziri wa biashara wa Ghana Hannah Tetteh akisema kuwa lengo la sheria hiyo ni kuyalinda maslahi ya wafanyabiashara wazalendo.Lakini sheria hiyo imeshasababisha mvutano baina ya Ghana na nchi nyingine za Afrika magharibi kama Nigeria. Gazeti la "die tageszeitung limewanukuu wabunge wa Nigeria wakitaka nchi yao ivunje uhusiano wa kibalozi na Ghana.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" wiki hii linakumbusha juu ya historia ya Ujerumani barani Afrika. Linakumbusha juu ya ukoloni wa Ujerumani katika Tanganyika ambayo leo inaitwa Tanzania. Ujerumani pia ilikuwa na makoloni, kama Togo na Kamerun . Lakini gazeti la "Der Tagesspiegel" linakumbusha hasa juu ya Namibia ambako maalfu ya watu wa kabila la Waherero na wa Nama waliangamizwa na Wajerumani kwenye mapambano ya "Waterberg" mnamo mwaka wa 1904.Watu hao walikuwa wanapigania uhuru wa nchi yao.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linakumbusha juu ya mswada uliowasilishwa bungeni na chama cha mrengo wa shoto-die Linke kutaka mauaji hayo yatambuliwe kuwa ni ya halaiki, na watu wa Namibia walipwe fidia.Lakini mswada huo ulipingwa.

Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef