1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika bado yakabiliwa na uhaba mkubwa wa umeme

7 Septemba 2023

Mataifa ya Afrika yaliopo kusini mwa jangwa la Sahara yanakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa umeme. Hatua mbalimbali ikiwemo kuboresha njia za usambazaji wa umeme zinahitajika kuchukuliwa ili kurekebisha hali hiyo.

https://p.dw.com/p/4W5BF
Uganda | Solarenergie in Soroti
Picha: Isaac Kasmani/AFP/Getty Images

Takriban watu milioni 567 wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara hawana umeme, likiwa eneo lenye uhaba zaidi wa umeme duniani.

Hii inamaanisha kuwa karibu nusu ya watu katika bara hilo hawawezi kuwasha mataa kufanya kazi zao ya nyumbani, kuwasha feni ili kujipoza na joto kali au hata kuchaji simu zao za mkononi ili kufanya shughuli mbalimbali kama kuagiza mbolea.

Abubakar Sambo, mkurugenzi mkuu wa zamani wa Tume ya Nishati ya Nigeria, amesema inasikitisha mno kuona eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika limeachwa nyuma linapokuja suala la umeme wakati ambapo maeneo mengine kama vile bara la Asia na eneo la Mashariki ya Kati, yanakaribia kuwa na upatikanaji kamili wa umeme.

Kenia Nairobi Kibera Slum
Kibera, Kenya ambako 20% tu ya makazi ndiyo yenye umeme: (03.02.2023)Picha: Simone Boccaccio/ZUMA Wire/IMAGO

Sambo ameiambia DW kuwa upatikanaji wa umeme barani Afrika si jumuishi. Kwa maana mnamo mwaka 2021, zaidi ya watu wanne kati ya watano wanaoishi katika maeneo ya vijijini kusini mwa Jangwa la Sahara hawakuwa na umeme.

Soma zaidi: Tatizo kubwa la umeme laikumba Afrika Kusini

Ingawa mataifa mengi ya Kiafrika yanaongeza usambazaji wao wa umeme, uboreshaji huo hauendani na kasi ya ongezeko la watu katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya maendeleo ya nishati iliyochapishwa na kundi la mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia na Chama cha Nishati cha (IEA), jumla ya idadi ya watu wasio na umeme katika eneo hilo ilisalia takriban sawa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2011 hadi 2021.

Soma pia: Zimbabwe yatangaza kumalizika kwa mgao wa umeme

Katika eneo la Afrika Magharibi na Kati, ongezeko la idadi ya watu limezidi kasi ya maendeleo ya usambazaji wa umeme katika kipindi hicho cha miaka 10, na hivyo kuwaacha asilimia kubwa ya watu wakiwa gizani.

Uhaba wa umeme: Kikwazo cha maendeleo

Kenya Stromausfall
Mkazi wa Kenya akitumia taa lake la dharura baada ya kukosa umeme Agosti 26,2023Picha: Abdul Azim Sayyid/AP/picture alliance

Ukosefu wa umeme ni kikwazo kikubwa cha maendeleo iwe katika kupata elimu, huduma za afya au kupata kazi. Takriban nusu ya shule za msingi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara hazina umeme, hii ikiwa ni kulingana na utafiti wa UNESCO wa mwaka 2023.

Wakati huohuo Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limebaini kuwa vituo vya afya vitatu kati ya vitano havina umeme eneo hilo. Biashara haziwezi kustawi mahali ambapo hakuna umeme, na ukosefu wake pia hufanya iwe vigumu kwa nchi za Kiafrika kuzalisha nafasi za kazi au kuvutia uwekezaji.

Soma pia: Janga la kitaifa latangazwa Afrika Kusini kufuatia ukosefu wa umeme

Lakini pia, umeme unaotolewa mara nyingi hauaminiki na huwa wa gharama kubwa. Uhaba wa umeme unayakumba mataifa mengi ya Afrika. Kwa mfano, ni nchi 2 tu kati ya 11 Kusini mwa Afrika ambazo ni Angola na Botswana ndizo zilizoepuka na tatizo la kukatika kwa umeme katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Mwaka huu,  Afrika Kusini nchi yenye uchumi mkubwa zaidi wa viwanda barani Afrika, imeshuhudia kukatika kwa umeme hadi saa 10 kwa siku.

Hali kama hiyo imeshuhudiwa katika sehemu kubwa ya Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo karibu makampuni manne kati ya matano ikiwa ni sawa na 78%, yameripoti kukabiliwa na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara na kwa muda mrefu, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi duniani.

Umeme wa maji waongezeka Afrika, lakini ni zipi changamoto?

(DW)