Afghanistan kupatiwa msaada wa dola bilioni 16 | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.07.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Afghanistan kupatiwa msaada wa dola bilioni 16

Wafadhili wakuu duniani Jumapili (08.07.2012) wameahidi kuipatia Afghanistan msaada wa maendeleo wa dola bilioni 16 hadi kufikia mwaka 2015.

Rais Hamid Karzai akizungumza na mawaziri wa Ujerumani, Guido Westerwelle na Dirk Niebel.

Rais Hamid Karzai akizungumza na mawaziri wa Ujerumani, Guido Westerwelle na Dirk Niebel.

Wafadhili wamechuwaa hatua hiyo katika juhudi za kuizuwiya nchi hiyo kutumbukia tena kwenye machafuko wakati vikosi vya kigeni vitapokuwa vimeondoka nchini humo.Hata hivyo wafadhili hao wameitaka nchi hiyo kufanya mageuzi ya kupamabana na rushwa.

Kuchoshwa kwa wafadhili katika suala la kuendelea kutowa misaada na vita visivyokuwa na mwisho kumetowa pigo kwa jumuiya ya kimataifa ambapo haijulikani kwa muda gani itabidi iendelee kuisaidia nchi hiyo. Pia kuna wasi wasi juu ya suala la usalama iwapo msaada wa kifedha hautopatikana baada ya kuondoka kwa takriban vikosi vyote vya Jumuiya ya Kujihami ya NATO hapo mwaka 2014.

"Usalama wa Afghanistan hauwezi tu kupimwa kwa kutokuwepo kwa vita." Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton ameuambia mkutano wa kimataifa wa wafadhili mjini Tokyo.

Amesema " Inabidi upimwe kwa kuangalia iwapo watu wana ajira,kuna fursa  za uchumi, iwapo wanaamii kwamba serikali inakidhi mahitaji yao na iwapo usuluhishi wa kisiasa unasonga mbele na kufanikiwa".

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton akizungumza katika hafla ya Jamii ya Kiraia ya Afghanistan mjini Tokyo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton akizungumza katika hafla ya Jamii ya Kiraia ya Afghanistan mjini Tokyo.

Vita dhidi ya rushwa

Clinton pia amesisitiza umuhimu wa Afghanistan, mojawapo ya nchi zilizotopea rushwa duniani  kuchukua hatua kali za kupambana na rushwa na kuendeleza mageuzi.

Amesema wamekubaliana kwamba wanahitaji ushirikiano wa kiuchumi wa muda mrefu wa aina tafauti chini ya msingi wa maendeleo ya Afghanistan kukidhi malengo yake katika kupiga vita rushwa,kutekeleza mageuzi na kuwa na utawala bora.

Rais Hamid Karzai amekiri serikali yake inatakiwa kuchukuwa hatua zaidi za kupambana na rushwa lakini wakosoaji wake wanasema hachukuwi hatua za kutosha na wengine hata wanailaumu serikali moja kwa moja kwa kima kikubwa cha msaada kushindwa kuwafikia walengwa.

Benki Kuu ya Afghanistan imekadiria kwamba zinahitajika dola bilioni 6 kwa mwaka kwa ajili ya uwekezaji mpya kutoka kwa wafadhili wa kigeni ili kuendeleza ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha muongo mmoja.

Waafghani wakiwa katika shughuli za miradi ya maendeleo nchini mwao.

Waafghani wakiwa katika shughuli za miradi ya maendeleo nchini mwao.

Masharti kwa msaada

Maafisa wa serikali ya Marekani hawakutaja kima cha msaada wanaotarajiwa kuutowa,lakini wamesema serikali italiomba bunge la Marekani kuendelea kuuimarisha msaada huo hadi mwaka 2017, kulinganisha na kile ambacho serikali ya Marekani imekitowa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Msaada wa kila mwaka wa Marekani kwa Afghanistan umekuwa kati ya dola bilioni 1 muongo mmoja uliopita na kuongezeka hadi kufikia dola bilioni 4 mwaka 2010 .Kwa mwaka huu msaada huo uko katika kima cha dola bilioni 2.3.

Japani imeahidi kutowa msaada wa dola bilioni 3 kwa Afghanistan hadi kufikia mwaka 2016. Waziri wa mambo ya nchi za nje Koichiro Gemba amesema dola bilioni 2.2 za msaada huo zitakuwa ni ruzuku kwa miradi ya maendeleo katika nyanja  kama vile uwekezaji katika barabara na miundo mbinu.

Umoja wa Ulaya umesema utaendelea na ahadi zake za kutowa msaada wa euro bilioni 1.2 kwa mwaka lakini umeonya kwamba iwapo hakutapigwa hatua katika utawala wa sheria na haki za wanawake, itakuwa vigumu kuendelea na ahadi hizo.

Ahadi hizo za misaada zilizotolewa huko Tokyo mji mkuu wa Japani ni ziada ya dola bilioni 4.1 za Jumuiya ya Kujihami ya NATO na washirika wake kwa ajili ya kuvisaidia vikosi vya Afghanistan.

Wawakilishi kutoka takriban nchi 80  na mashirika ya misaada ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Benki Kuu na Benki ya Maendeleo ya Asia walihudhuria mkutano huo  wa misaada mjini Tokyo.

Afghanistan bado inaendelea kuwa mojawapo ya nchi tano maskini kabisa duniani.Imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha kwamba watoto wanakwenda shule na kuboresha kupatikana kwa huduma za matibabu ,lakini theluthi tatu ya wananchi milioni 30 wa Afghanistan hawajuwi kusoma na kuandika na mtu wa  kawaida hujipatia dola 530 tu kwa mwaka.

Mwandishi:Mohamed Dahman(RTR)

Mhariri:Iddi Ismail Ssessanga

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com