1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA:Watuhumiwa wa uhaini waachiwa

12 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCAV

Jaji mmoja nchini Ethiopia amewaachia waandishi wanane na watu wengine 17 waliodaiwa kuhusika na keshi ya uhaini iliyojumuisha wafuasi 100 wa upinzani.Kesi hiyo imezua utata katika jamii ya kimataifa na kuelezwa kuwa ina misingi ya kisiasa.

Jaji Adil Ahmed aliiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha madai ya uhaini dhidi ya wahusika 25 na kuamuru polisi kuwaachilia papo kwa papo.Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka mkuu Shimeles Kemal aliyezungumza na shirika la habari la Reuters,uamuzi huo unazua utata na huenda wakaomba rufaa katika masuala kadhaa.

Jaji huyo aidha aliwaagiza viongozi wa chama kikuu cha Upinzani Coalition for Unity and Democracy kujitetea katika kesi dhidi yao.Mpaka sasa wanasiasa hao wanaripotiwa kukataa kushirikiana na mahakama kwa madai kuwa kesi hiyo ina misingi ya kisiasa.

Waandishi wa habari na wanaharakati wa kisheria walishtakiwa mwezi Disemba mwaka 2005 kwa kosa la uhaini,kuchochea ghasia vilevile kujaribu kusababisha mauaji ya halaiki.Mashtaka hayo yalitoplewa kufuata ghasia zilizozuka mahala tofauti na kusababisha vifo vya takriban watu 80 pale waandamanaji na majeshi ya usalama walipopambana.Hii ilifanyika mwaka 2005 baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa yaliyodaiwa kuwa na ila na upande wa upinzani.

Kati ya watu 131 walioshtakiwa,45 wameachiwa na wengine 36 waliosalia wanashtakiwa bila kuwepo.Kulingana na sheria nchini Ethiopia,washtakiwa waliohukumiwa hupata adhabu ya kifo endapo shtaka la kusababisha mauaji ya halaiki linathibitishwa na mahakama.