1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA:Waasi wa ONLF kutafutiwa suluhu

29 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBUi

Umoja wa Mataifa unapanga kupeleka ujumbe kuchunguza eneo la Ogaden nchini Ethiopia lililo na waasi wanaotaka kujitenga.Waasi hao wamesababisha vifo vya watu 74 huku serikali ikitia juhudi zote kuwasaka.Ujumbe huo unalenga kuchunguza madai ya kukiukwa haki zao za binadamu ya waasi hao vilevile makundi ya kutetea haki za binadamu aidha mahitaji yao ya maji,chakula na huduma za afya.Eneo la Ogaden lina wakazi walio na asili ya Kisomali na ujumbe huo unaanza shughuli zake mwishoni mwa mwezi huu.

Eneo hilo limekuwa likitazamwa sana katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni tangu serikali kuanzisha kampeni ya kuwafurusha waasi wa Ogaden National Liberation Front, ONLF baada ya kushambulia kiwanda cha mafuta kinachoendeshwa na Wachina mwezi Aprili.

Kulingana na makundi ya kutetea haki za binadamu jeshi liliteketeza nyumba,kukamata mifugo aidha kuwapiga risasi raia walipokuwa wakiwasaka waasi wa ONLF.Kundi la ONLF linataka umiliki mkubwa zaidi katika eneo hilo linaloaminika kuwa na mafuta na gesi.

Kwa mujibu wa Waziri mKuu wa Ethiopia Meles Zenawi waasi wa ONLF ni magaidi wanaofadhiliwa na nchi jirani ya Eritrea iliyo adui wao.

Kundi la ONLF kwa upande wake linapokea vizuri hatua ya Umoja wa mataifa kama juhudi za kujaribu kutafuta ufumbuzi kwa tatizo hilo la Ogaden.Ujumbe huo unawahusisha wafanyikazi kutoka Shirika la Kutetea haki za binadamu la umoja wa mataifa vilevile mashirika ya misaada yanayohusika na huduma kwa watoto,usambazaki wa chakula na huduma za matibabu.