1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA : Eritrea yashutumiwa kuteka nyara watalii

4 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCMf

Afisa mwandamizi wa serikali ya Ethiopia hapo jana amewashutumu wanajeshi kutoka nchi jirani ya Eritrea kwa kuliteka nyara kundi la watalii wa Uingereza ambao magari yao ya utalii yamepatikana yakiwa yameteketezwa karibu na mpaka.

Hali ya wasi wasi imekuwa ikiongezeka juu ya usalama wa wafanyakazi hao wa ubalozi wa Uingereza na jamaa zao ambao wametoweka hapo Alhamisi pamoja na Waethopia 13 katika jimbo la jangwa la Afar lilioko mbali kabisa kaskazini mashariki mwa Ethiopia.

Rais wa jimbo hilo Ismail Ali Sero ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hadi sasa wanachojuwa tu ni kwamba Waingereza hao watano wamechukuliwa na Shabia akimaanisha wanajeshi wa Eritrea na kupelekwa nchini Eritrea.Amesema wameweza kujuwa hayo kwa sababu Waethiopia watatu waliokuwa wametekwa wakiwa na kundi hilo la watalii wameachiliwa na kuthibitisha hayo.

Eritrea imekanusha madai hayo.

Wakati huo huo kuna repoti kwamba kundi la raia saba wa Ufaransa ambao walikuwa hawajulikani walipo wako salama ingawa serikali ya Ufaransa haikuthibitisha taarifa hiyo.