1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

2024: Mwaka wa uchaguzi barani Afrika

Saumu Mwasimba
8 Januari 2024

Mwaka 2024 huenda utakuwa ni mwaka wenye mambo mengi ya kusisimua kwa bara la Afrika, zikitarajiwa kufanyika chaguzi katika nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/4ayGJ
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Pavel Bednyakov/RIA Novosti/AP/dpa/picture alliance

Wataalamu wanasema uchumi wa bara hilo unakuwa, licha ya kukosekana uthabiti katika maeneo mengi ya kanda hiyo. Ripoti ifuatayo inayatazama masuala kadhaa yakumulikwa katika bara la Afrika mwaka huu wa 2024. 

Katika kanda ya magharibi mwa Afrika, maandamano tayari yameshazuka nchini Senegal kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Ujao wa Februari. Rais Macky Sall amejiondowa kwenye kinyang'anyiro hicho, lakini amemteuwa waziri mkuu Amadou Ba kuingia kwenye uchaguzi huo kurithi nafasi yake.

Kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko ambaye ni mwanasiasa machachari aliyewahi kugombea urais mwaka 2019 na kushika nafasi ya tatu, amezuiwa kugombea uchaguzi huo kufikia hivi sasa. Aliondolewa kwenye orodha ya wagombea baada ya kukutwa na hatia na kuhukumiwa miaka miwili jela, mwezi Juni mwaka jana, kwa makosa ya kupotosha vijana kimaadili. Sonko hakuweko mahakamani wakati hukumu hiyo ilipotolewa.

Soma pia:  Afrika kugeukia nishati ya nyuklia kuzalisha umeme?

Mwanasiasa huyo na timu yake ya wanasheria wanasema kesi zilizoko mahakamani dhidi ya Sonko ni sehemu ya juhudi za kumuharibia safari yake ya kisiasa. Lakini ukiitazama hali ya kisiasa nchini Afrika Kusini, inaelezwa kwamba hali sio nzuri kwa chama cha African National Congress, ANC.

Wako wanaobashiri kwamba chama hicho kitapoteza kwa kiasi kikubwa. Nchi hiyo itaingia kwenye uchaguzi mnamo mwezi Mei na wachambuzi wengi hawana uhakika ikiwa chama cha ANC kitaweza kutetea wingi wake bungeni.

Kura za maoni zinaonesha chama hicho kinachoongozwa na Rais Cyril Ramaphosa kinaweza kushuka chini ya asilimia 50 kwa mara ya kwanza tangu ulipofanyika kwa mara ya kwanza uchaguzi huru mnamo mwaka 1994. Ikiwa hivyo ndivyo itakavyotokea hapana shaka chama hicho kitalazimika kuunda serikali ya mseto na vyama vidogo ili kiendelee kubakia madarakani.

Ukosefu wa ajira ni pasua kichwa Afrika Kusini

Maandamano ya kumtaka Rais Cyril Ramaphosa ajiuzulu
Maandamano ya kumtaka Rais Cyril Ramaphosa ajiuzuluPicha: Alet Pretorius/REUTERS

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa, Fredson Guilengue, kutoka taasisi moja ya Afrika Kusini ambayo ina mafungamano na chama cha kisiasa cha mrengo wa kushoto cha siasa za mitizamo ya ujamaa, anasema serikali nyingi katika eneo zima la kusini mwa Afrika, iwe ni Msumbiji, Zimbabwe au Afrika Kusini zimeundwa chini ya misingi ya kupambana na sera za ukoloni.

Lakini kizazi cha hivi sasa hakina mafungamano na mambo yaliyopita na matarajio yao ni kuwaona viongozi wao wakifanya mambo tofauti. Nchini Afrika Kusini kiasi asilimia 70 ya watu hawajaridhika na utekelezwaji wa demokrasia nchini humo, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na taasisi ya Afrobarometer. Waafrika Kusini walio wengi wanalitazama suala la ukosefu wa ajira ni muhimu zaidi katika uchaguzi ujao likifuatiwa na suala la uhalifu na usalama, umeme, maji na rushwa.

Soma pia: Urusi inataka nini Afrika? 

Kudumaa kwa hali ya uchumi pamoja na kuweko taswira ya kutoaminiana ndani ya serikali ni mambo yaliyoongeza mivutano katika nchi hiyo, na hali ni hivyo hivyo nchini Msumbiji ambako wananchi wanajaribu kuupigia upatu zaidi upinzani.

Ikumbukwe kwamba mwaka jana mwezi Oktoba ulifanyika uchaguzi wa serikali ya mitaa na chama cha upinzani Renamo kilikishutumu chama tawala Frelimo kwa kufanya udanganyifu katika uchaguzi uliokipa ushindi chama hicho tawala wa viti 64 kati ya 65. Vurugu zilizuka baada ya kutangazwa matokeo na vifo vya watu kadhaa vilitokea.

Kiswahili lugha inayoliunganisha bara la Afrika

Kanda ya Afrika Magharibi hata hivyo bado ndiyo inayobakia kuwa tete. Hali ya wananchi kutoridhika na tawala zilizopo madarakani inaweza kusababisha mabadiliko ya kuingizwa madarakani vyama vya upinzani katika nchi kama Ghana, ambayo itafanya uchaguzi mwezi Desemba. Hakuna uwezekano wa utawala wa kijeshi nchini Mali kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia hivi karibuni, japo uchaguzi umepangwa kufanyika mwezi Februari mwaka huu.

Soma pia: Xi akataa miradi isiyo na tija Afrika 

Kitengo cha uchunguzi cha gazeti la The Economist kimeonesha kwamba kuna hatari iliyoongezeka kwa ujumla ya kupunguwa ushawishi wa wanaoshikilia wingi bungeni kwa mfano katika nchi za Madagascar, Algeria na Tunisia, hali ambayo itasababisha kuweko matatizo ya uongozi na kuchochea machafuko.

Nchi nyingi zinaonesha kupiga hatua kiuchumi katika bara hilo kwa mujibu wa gazeti la The Economist, ingawa kwa mujibu wa waatalamu, suala la kupunguziwa madeni litabakia kuwa ajenda kuu kwa nchi kama Msumbiji na nyingine nyingi katika bara hilo.