Zu Guttenmberg awasili Kundus | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Zu Guttenmberg awasili Kundus

Ujerumani kuengeza vikosi Afghanistan.

Waziri wa ulinzi zu Guttenmberg

Waziri wa ulinzi zu Guttenmberg

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenmberg,amewasili leo asubuhi Kundus, kaskazini mwa Afghanistan, kujionea binafsi hali ya mambo ilivyo. Itakumbukwa kwamba, hapo Septemba 4,kwa amri ya amirijeshi wa kijerumani katika eneo hilo, moja kati ya malori 2 ya shehena ya mafuta yaliotekwanyara na watalibani lilishambuliwa kwa mabomu.Watu 142 wakauwawa.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani zu Guttenmberg alifunga jana safari yake ya kwanza nchini Afghanistan na Kundus ni kituo cha mwisho cha ziara yake kabla hakurejea Berlin leo jioni. Ziara yake inafanyika chini ya ulinzi mkali na pale ndege yake ya helikopta ilipotua Kundus mapema asubuhi ya leo ,ndege maalumu ya ukaguzi wa anga isio na binadamu ilirushwa angani.

Alipovitembelea vikosi vya Ujerumani huko Kundus alikowasili bila tangazo la kabla,zu Guttenmberg,alisema kwa hali iliochafuka ya usalama huko Kundus ,anapanga kuongeza wazi idadi ya wanajeshi wa Ujerumani-Bundeswehr- sehemu hiyo.

Zu Guttenmberg, aliongeza kusema kwamba, kati ya Januari mwakani,kikosi zaidi cha Bundeswehr, kikiwa na jumla ya askari 120 kitapelekwa katika eneo hilo la machafuko.Kikosi hicho kitaiimarisha kile cha wanajeshi 450 wa Ujerumani waliopo huko tayari .Hiki ni kikosi ambacho pakizuka balaa na watalibani kimeruhusiwa kufyatua risasi.

Kabla hakufunga safari kurejea leo Berlin, waziri wa ulinzi wa Ujerumani alisema, "Hapa sio kila kitu ni cha utulivu na cha furaha ili kustarehe." Katika kazi ya kuijenga upya Afghanistan, hivi sasa kuna jumla ya askari 1.100 wanaotumika huko Kundus na kati ya hao, 1000 ni kutoka Ujerumani na 100 ni wabelgiji.

Kabla kuwasili leo Kundus, waziri wa ulinzi wa Ujerumani, aliwaambia wanajeshi wa Ujerumani huko Masar-i-Sharif,kaskazini mwa Afghanistan, kwamba Afghanistan, itaendelea kuwashughulisha kwa muda zaidi unaokuja .Kwahivyo, Afghanistan nayo inapaswa kuchangia binafsi katika ulinzi wake.

zu Guttenmberg akaongeza kusema kwamba, serikali ya Ujerumani, itaiwekea wazi serikali ya rais Hamid Karzai kwamba, mdomo mtupu hautoshi.

Siku 1 tu baada ya ziara ya waziri huyo wa Ujerumani mjini kabul, mji mkuu wa Afghanistan,lilifanyika mapema hii leo shambulio kali la mtu aliejiripua mjini humo.

Mkuu wa Idara ya kupambana na uhalifu ya mji mkuu huo Kabul,Sayed Abdul Ghafar, aliarifu kwamba , waafghani 3 walijeruhiwa katika mripuko huo kwenye kambi ya wanajeshi ,mashariki mwa Kabul.Hiyo ni ile kambi ya Camp Phoenix ambayo hutumiwa na vikosi vya kigeni.

Mswandishi: Ramadhan Ali/DPA

Uhariri: Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com