1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kuhesabu kura laendelea Mali

Amina Mjahid
30 Julai 2018

Kura zinaendelea kuhesabiwa Mali baada ya kufanyika uchaguzi utakaoamua ikiwa rais Ibrahim Boubacar Keita atashinda muhula wa pili huku kukiwa na vurugu zilizoshamiri tangu Keita aingie madarakani miaka mitano iliyopita

https://p.dw.com/p/32Ilj
Mali Wahlen
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Zoezi hilo la kuhesabu kura lilianza mjini Bamako baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa kumi na mbili jioni hapo jana. Katika shule moja ya msingi iliotumiwa kama kituo cha kupigia kura maafisa walijumuisha matokeo katika ubao wa kuandikia.

Hata hivyo matokeo rasmi bado hajayatolewa na wagombea wamezuiwa kutangaza chochote kabla ya matokeo  rasmi kutangazwa. Watu milioni 8 ndio walioandikishwa kupiga kura na wagombea katika uchaguzi huu wanajumuisha wafanyabiashara, mwanasayansi  na mwanamke mmoja.

Mali Wahlen
Wapiga kura wakiwa nje ya vituo vya kupigia kura Mali Picha: Imago/Le Pictorium/N. Remene

Wagombea hao zaidi ya 20 wanapigania nafasi ya urais katika taifa kubwa lililo eneo la Jangwa la Sahara lililoharibiwa na waasi wa kituareg na mashambulizi ya wanamgambo wa kiislamu katika maeneo yake ya Kaskazini na maeneo ya kati tangu kulipofanyika uchaguzi uliopita mwaka 2013.

Katika maeneo mengine ya Mali, uchaguzi haukufanyika kutokana na ukosefu wa usalama huku Mkuu wa Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya Cecile Kyenge ameihimiza serikali nchini humo kuweka wazi maeneo ambayo uchaguzi haukufanyika ili kuwaondolea wasiwasi wagombea.

Ukosefu wa usalama wazuia zoezi la uchaguzi kufanyika katika baadhi ya maeneo Mali

Katika mkutano na waandishi habari hapo jana jioni, Mkurugenzi wa kampeni ya mgombea Soumaila Cisse, mwenye umri wa miaka 68 ambaye ndie mshindani wa karibu wa  rais Keita, amekadiria kuwa vituo vya kupigia kura 644 kati ya 23,000 havikuweza kufunguliwa wakati wa zoezi la uchaguzi kutokana na ukosefu huo wa usalama.

Mali Kämpfer der islamistischen Gruppe Ansar Dine
Baadhi ya wanamgambo wa Kiislamu Kaskazini mwa MaliPicha: Getty Images/AFP/R. Hien

kilomita 1000 kutoka Kusini Magharibi mwa mji wa Bamako Hama Diallo aliye na miaka 32 anasema matumaini yake ni kuona siku za usoni zilizo salama. Ameongeza kuwa anatumai rais atakaechaguliwa ataweka kipaumbele katika masuala ya Usalama.

Miaka mitatu iliyopita mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi yamezidi nchini Mali na kuongeza mara mbili vifo vitokanavyo na vurugu hii ikiwa ni kulingana na tovuti ya shirika la kiraia Malilink.

Wanamgambo wamesambaa kutoka Kaskazini hadi maeneo ya kati na kulenga mji mkuu Bamako wakati watu waliojihami kwa bunduki waliposababisha vifo vya watu 20 wapovamia hoteli moja mwaka 2015.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu