Zimbabwe yaadhimisha miaka 27 ya uhuru | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.04.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Zimbabwe yaadhimisha miaka 27 ya uhuru

Zimbabwe leo inaadhimisha miaka 27 tangu ijipatie uhuru wake, lakini nchi hiyo inakabiliwa na hali mbaya ya uchumi na mivutano ya kisiasa ambayo imeigeuza nchi iliyokuwa zamani kioo cha bara la Afrika na kuwa nchi iliyotengwa na jamii ya kimataifa.

Rais Robert Mugabe

Rais Robert Mugabe

Kauli mbiu ya mwaka huu katika kusherehekea miaka 27 ya uhuru wa taifa hilo lililokuwa zamani koloni la Uingereza ni - Kuungana Dhidi ya Vikwazo – ishara dhahiri ya kupinga vikwazo vilivyowekwa na nchi za umoja wa ulaya na Marekani dhidi ya utawala wa rais Robert Mugabe kwa madai kwamba uchaguzi wa mwaka 2004 uliompatia ushindi uligubikwa na kasoro nyingi.

Mugabe mwenye umri wa miaka 83 na ambae ameitawala Zimbabwe tangu ilipopata uhuru wake leo hii ataongoza sherehe hizo katika uwanja mashuhuri mjini Harare ambako kwa mara ya kwanza sherehe za uhuru wa nchi hiyo ziliadhimishwa.

Maadhimisho ya uhuru wa Zimbabwe pia yanatarajiwa kufanyika katika sehemu mbali mbali za nchi hiyo.

Lakini wachambuzi wamebashiri kwamba kutokana na hali duni ya maisha na juhudi za serikali za kuwasaka na kuwaadhibu maadui wa serikali hiyo, siku hii imepoteza umuhimu wake.

Takura Zhangaza mchambuzi wa maswala ya kisiasa nchini Zimbabwe anasema watu wengi wanapata shida na hawana furaha ya kusherehekea na wakati huo huo sherehe za kisiasa haziwezi kutatua jambo lolote nchini Zimbabwe.

Nchi hiyo iliyo katika eneo la Kusini mwa Afrika na yenye wananchi milioni 13 iliheshimiwa na kuitwa kikapu cha mkate hapo zamani lakini sasa inakabiliwa na kiwango cha juu cha maisha, gharama ya maisha imepanda hadi kufikia asilimia 1,730 na ajira zimekuwa adimu kupatikana kwani kiwango cha asilimia 80 ya watu hawana ajira.

Uhusiano wa serikali ya rais Robert Mugabe na mataifa ya ulaya uligonga mwamba mwezi uliopita pale kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC alipokamatwa na kuzuiliwa pamoja na wenzake walipojaribu kuongoza maandamano ya kupinga utawala wa rais Mugabe.

Lawama zilitolewa kutoka pembe zote za dunia na rais Mugabe akajibu kwa kutishia kuwafukuza wanadiplomasia wa kigeni kutoka nchini mwake na kusisitiza kuwa Tsvangirai angepaswa kujilaumu mwenyewe.

Hali ilikuwa tafauti kabisa miaka 27 iliyopita nchini Zimbabwe wakati rais Mugabe alipopata umaarufu na sifa tele kwa hatua yake ya kutangaza suluhu na weupe wachache mara tu walipoikabidhi nchi hiyo uhuru baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kiranja wa bunge la Zimbabwe Rugare Gumbo anasema kwamba siku ya uhuru inafaa kupewa umuhimu licha ya kuwa Zimbabwe inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.

Ameongeza kusema kuwa kwa sasa raia wa Zimbabwe wangepaswa kujivunia uwezo wa kujiamulia mambo tafauti na hapo kale ilipokuwa uwezo huo ulikuwa mikononi mwa weupe wachache tu ambapo raia weusi hawakuruhusiwa hata kukanyaga katikati ya mji.

Rais Robert Mugabe analaumu hali mbaya ya uchumi nchini mwake kuwa imesababishwa na mpango wa nchi za magharibi unaotaka ang’olewe madarakani.

Kasisi mbishi wa kanisa katoliki nchini Zimbabwe Pius Ncube anasema…. namnukuu….Mugabe ana kiu cha kubakia madarakani hata ikiwa gharama yake ni kuuharibu uchumi au kuiangamiza Zimbabwe kabisa….mwisho wa kumnukuu.

Nchi za magharibi zimekanusha madai ya rais Mugabe na zimesisitiza kwamba zinatetea kurudisha demokrasia nchini Zimabwe.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com