Zimbabwe: Mnangagwa ameapishwa kuwa rais mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Zimbabwe: Mnangagwa ameapishwa kuwa rais mpya

Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 amekula kiapo ya kuwa rais mpya wa Zimbabwe.

Emmerson Mnangagwa ndiye rais mpya wa Zimbabwe. Mnangagwa ameapishwa muda mchache ambao umepita hivyo amechukua hatamu ya rais kutoka kwa Robert Mugabe aliyejiuzulu baada ya kuitawala nchi hiyo kwa miaka 37.

Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75 amekula kiapo ya kuwa rais wa Zimbabwe.

Shangwe, muziki, densi na nyimbo za sherehe zimeutawala uwanja huo mjini Harare wakati ya sherehe ya kuapishwa kwa Mnangagwa.

Sherehe hiyo inayoendelea imehudhuriwa na maelfu kwa maelfu ya watu pamoja na viongozi kadhaa, akiwemo kiongozi wa vuguvugu la upinzani la Democratic Change Morgan Tsvangirai.

SADC yaahidi kushirkiana na serikali ya Mnangagwa

Jeshi likiandaa gwaride la heshima katika sherehe ya kuapishwa kwa Mnangagwa

Jeshi likiandaa gwaride la heshima katika sherehe ya kuapishwa kwa Mnangagwa

Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC imesema iko tayari kushirikiana kwa karibu na kiongozi mpya wa Zimbabwe na serikali yake. Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma hajahudhuria sherehe hizo. Hata hivyo alituma udhuru.

Baadhi ya Wazimbabwe, wameelezea furaha yao, na matumaini makubwa waliyo nayo kwa Mnangagwa. Hizi ni baadhi ya kauli za Wazimbabwe ambao wameelezea hisia zao: "Ninayo furaha tele kuwa na rais mpya. Siwezi kukuelezea jinsi nilivyo na furaha. Wow! Inapendeza sana! "Hii ndiyo siku ya furaha zaidi katika maisha yangu na ninataka kuisifia na kuithamini siku hii."

Usalama umeimarishwa vilivyo, huku maafisa wa polisi na jeshi wakishika doria.

Robert Mugabe aliyeitawala nchi hiyo kiimla kwa miaka 37, alijiuzulu mapema wiki hii, baada ya jeshi kuchukua madaraka wiki iliyopita pale alipomfuta kazi makamu wake Mnangagwa.

Mugabe ahakikishiwa usalama

Hapo awali, Mnangagwa alimhakikishia Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 93 ulinzi kamili pamoja na familia yake kama raia wa Zimbabwe. Mugabe amepewa kinga ya kutoshitakiwa.

Wafuasi wa Mnangagwa mjini Harare

Wafuasi wa Mnangagwa mjini Harare

Aidha amempongeza kwa matayarisho ya kuwezesha kuapishwa kwake leo. Hayo yalitangazwa mapema leo na shirika la habari la serikali nchini humo Herald News.

Mnangagwa aliyerejea Zimbabwe wiki hii baada ya kuondoka alipofutwa kazi na Mugabe, alisema kuwa Zimbabwe inashuhudia demokrasia mpya na kamili. Hata hivyo wakosoaji wanahoji kuwa yeye ni mwanachama wa ZANU-PF mwenye misimamo mikali aliyepata madaraka kupitia mapinduzi mbadala ya kijeshi.

Anafahamika kama "Mamba" kufuatia ukatili wake na anadaiwa kusimamia mauaji yaliyofanywa na wanajeshi miaka ya 1980 na mwaka 2008 wakati wa ghasia za kisiasa wakati Mugabe nusura ashindwe katika uchaguzi wa rais.

Wakati haya yakifanyika, aliyekuwa waziri wa fedha nchini humo, Ignatius Chombo ambaye alikuwa akishikiliwa na jeshi tangu wiki iliyopita jeshi lilipochukua madaraka, amekabidhiwa kwa maafisa wa polisi.

Wakili anayemwakilisha amesema hayo na kuongeza kuwa yupo hospitalini kwa sasa kwa matibabu, japo hakufafanua vipi anaugua. Profesa Lovomore Madhuku amesema Chombo atafikishwa mahakamani na labda akabiliwe na mashtaka ya kutumia vibaya mamlaka ya ofisi yake.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com