1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zilzala ya kisiasa katika jimbo la North Rhine Westphalia baada ya uchaguzi wa bunge la jimbo

Oumilkher Hamidou10 Mei 2010

Eti kweli yaliyotokea miaka mitano iliyopita baada ya uchaguzi wa jimbo hili,yanaweza kutokea na safari hii ,pia uchaguzi mkuu utakapoitishwa?Wanajiuliza wahariri

https://p.dw.com/p/NKIH
Mwenyekiti wa chama cha SPD katika jimbo la North Rhine Westphalia bibi Hannelore KraftPicha: AP

Uchaguzi katika jimbo lenye wakaazi wengi zaidi nchini Ujerumani ndio mada iliyohanikiza magazetini hii leo.

Tuanze na gazeti la "Allgemeine Zeitung la mjini Mainz linaloandika:

Hatimae mtu anaweza kutathmini matokeo ya uchaguzi wa jimbo la North Rhine Westphalia kua ni kura ya kutokua na imani na serikali ya Angela Merkel.Sawa na inavyokuwa tetemeko la ardhi linapopiga,na zilzala hii pia ya uchaguzi matokeo yake hayakadiriki.Kimoja lakini ni dhahir:Kuanzia leo wanasocial Democratic wana usemi mjini Berlin.Ujerumani inajikuta katika kizungumkuti cha kuwa na serikali kuu ambayo kimsingi haiko tena.

Gazeti la Berlin Zeitung linakwenda mbali zaidi na kuandika:

Kwa kupoteza wingi wa viti katika bunge la mjini Düsseldorf kansela Merkel amepoteza pia wingi wa viti katika baraza la wawakilishi wa majimbo-Bundesrat.Inamaanisha kwamba shirikisho la jamhuri ya Ujerumani kuanzia sasa linaongozwa japo si moja kwa moja na serikali ya muungano wa vyama vikuu.Anachokitaka Westerwelle,Merkel hatolazimika sana kukizingatia.Lakini kile Gabriel na Steinmeier watakachokitaka ndicho kitakachofafanua mipaka ya uwezo wake wa kuamua.

Gazeti la mji wa kaskazini la "HANNOVERSCH ALLGEMEINE linalinganisha hali namna ilivyokua baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na kuandika:

Miaka mitano iliyopita Rüttgers ndie aliyesababisha kuporomoka Gerhard Schröder na kusafisha njia ya kuweza kuingia madarakani serikali ya kansela Angela Merkel na makamo wake Guido Westerwelle.Miezi minane baada ya ushindi wa muungano wao, vyama ndugu vya CDU/CSU na waliberali wa FDP hawajafanikiwa kujitokeza kama serikali yenye kufanya kazi ipasavyo.Bado hawakubaliani,hata katika masuala muhimu,wanazusha hisia kana kwamba wanavuta wakati na matatizo wanajaribu kuyaficha.Serikali hii inataka kucheza na Ujerumani.Jee hali itabadilika sasa?Uwezekano upo kuona kisa cha Düsseldorf kikiwazungusha kichwa wanaoongoza muungano mjini Berlin.

Gazeti la "OLDENBURGISCHE VOLKSZEITUNG" linajaribu kuchambua sababu zilizopelekea kushindwa muungano wa nyeusi na manjano mjini Düsseldorf.Gazeti linaendelea kuandika:

Matokeo ya uchaguzi katika jimbo la North Rhine Westphalia ni balaa la mara dufu kwa CDU na FDP.Muungano wa nyeusi na manjano umepigwa kumbo katika maeneo ya mito Rhine na Ruhr-baada ya mhula mmoja tuu.Na matokeo hayo ya uchaguzi ni onyo pia kwa serikali ya muungano kaatika eneo la mto Spree mjini Berlin.Kishindo chote hicho cha chama cha CDU kimeshadidiwa na mlolongo wa kashfa zinazokigubika chama hicho katika jimbo la NORTH Rhine Westphalia.Ndio maana anaebebeshwa zaidi jukumu la pigo hilo la kihistoria si mwengine isipokua mwenyekiti wa CDU katika jimbo la NRW na ambae pia ni waziri mkuu Jürgen Rüttgers.

Gazeti la "WESTFÄLISCHE NACHRICHTEN" la mjini Münster linajiuliza muungano wa aina gani utaingia madarakani mjini Düsseldorf? Gazeti linaendelea kuandika:

Haijulikani bado nani ataongoza serikali katika jimbo la North Rhine Westphalia.Walinzi wa mazingira wanaojivunia ushindi dhahiri watajua namna ya kuwazuwia lakini SPD na CDU wasiunde serikali ya muungano.Wanaweza kuridhia wafuasi wa mrengo wa shoto-Di Linke wajiunge serikalini.Suala ni kama bibi Hannelore Kraft ataridhia.

Mwandishi :Hamidou Oummilkheir /DPA

Imepitiwa na:Mohammed Abdul-Rahman