1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Papa Benedikti nchini Lebanon

Mohamed Abdulrahman15 Septemba 2012

Awataka waumini wa dini zote kuishi kwa amani na maridhiano miongoni mwa Walebanon

https://p.dw.com/p/169f4
Pope Benedict XVI greets faithful from his Pope Mobile upon arrival at the Baabda Presidential Palace near Beirut September 15, 2012. REUTERS/Mohamed Azakir (LEBANON - Tags: POLITICS RELIGION)
Papa BenediktiPicha: Reuters

Kiongozi  wa Kanisa Katoliki Duniani Benedikti XV1, amewataka Wakristo na Waislamu katika Mashariki ya Kati kuunda  jamii  iliyostawi ya watu wa dini zote ambapo utu wa kila mtu na haki ya kuabudu kwa amani itahakikishwa. Papa alikuwa akizungumza na Viongozi wa kisiasa na kidini, katika siku ya pili ya ziara yake  ya siku tatu nchini Lebanon Jumamosi.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani alisisitiza kwamba  umma lazima ukatae ulipizaji kisasi, utambuwe makosa yake na kusameheana.

Maelfu ya watu wengi wao wakiwa Wakristo ikiwemo idadi kubwa ya watoto, walijipanga katika barabara inayoelekea kasri la Rais, asubuhi ya jua lililochomoza ili kumuona Papa Benedikti XV1 wakati akielekea Ikulu. Miongoni mwao walikuwemo Wamisri, Wairaki, Wajordan na Wapalestina, waliofika  kujionea ziara yake ya  kwanza nchini Lebanon tangu ile ya  John Paul II mwaka 1997.

Pope Benedict XVI waves from the podium next to Lebanon's President Michel Suleiman upon his arrival at Beirut's airport September 14, 2012. Pope Benedict appealed for a stop to arms imports to Syria on Friday, saying it would help end the civil war there, and said the Arab Spring was a positive "cry for freedom" as long as it included religious tolerance. REUTERS/Stefano Rellandini (LEBANON - Tags: RELIGION POLITICS)
Papa Benedikti na Rais SleimanPicha: Reuters

Papa Benedikti mwenye umri wa miaka 85 akitembea  na gongo alikutana kwanza na  Rais Michel Sleiman ambaye ni mkristo wa madhehebu ya  Maronite. Baadae kabla ya kuwa na mazungumzo na viongozi wa Kiislamu alionana na na Waziri Mkuu Nagib Mikati, Muislamu wa madhehebu ya Sunni na Spika wa Bunge Nabih Berri,Mshia. Lebanon ina utaratibu wa kijadi ambapo nafasi tatu za Uongozi wa juu hutengwa kwa  watu wa jamii hizo tatu za kidini. Pamoja na umati uliomlaki Kiongozi huyo kuwa mkubwa , ulinzi  pia ulikuwa mkali.

Bodyguards escort the Pope Benedict XVI greeting faithful from his Pope Mobile, upon arrival at Baabda Presidential Palace near Beirut, September 15, 2012. Pope Benedict is in Lebanon on a three-day visit. REUTERS/Hasan Shaaban(LEBANON - Tags: POLITICS RELIGION)
Ulinzi mkali wakati wa ziaraPicha: Reuters

Papa Benedikti alisema wale wanaowajibika kuishi kwa amani hawana budi pia kubadili nyoyo zao na  ni pamoja na kukataa ulipizaji kisasi akiongeza kwamba amekuja na  risala ya amani katika sehemu hii ya dunia na kwengineko Mashariki ya kati.  Akauliza ,"kwanini Mwenyezi Mungu amezichagua ardhi hizi, na kwanini maisha ya wakaazi wake ni ya misukosuko ?

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani akajibu kwa kusema , anafikiri Mungu alizichagua ardhi hizo, ili ziwe ni mfano na ushahidi mbele ya dunia kwamba kila mwanamme au mwanamke anawajibu wa kujitolea kwa ajili ya amani na maridhiano. Moyo huo ni sehemu ya mpango wa Mwenyezi Mungu kuhusu roho na ameuweka ndani ya roho ya binaadamu.

Alisema amani inawezekana tu pakiweko na jamii iliyoungana yenye Umoja na kama tunataka amani  basi hatuna budi kuyalinda maisha, alisema Papa Benedikti. Ratiba yake ya mwisho Jumamosi ni kukutana na vijana wa Lebanon Wakristo na wengineo, karibu na  kijiji cha Bkerke. Papa Benedikti XV1 atarejea Roma kesho baada ya misa ya wazi mjini Beirut.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,afp

Mhariri: Mohamed Dahman