Ziara ya Papa Afrika | NRS-Import | DW | 18.03.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Ziara ya Papa Afrika

Wataalam wa afya wamekosoa msimamo wa Kiongozi wa kanisa Katoliki, Papa Benedict wa 16, kuwa matumizi ya kondom yanachangia pakubwa kuambukizwa kwa virusi vya ukimwi.

Kiongozi wa kanisa Katoliki, Papa Benedict wa 16.

Kiongozi wa kanisa Katoliki, Papa Benedict wa 16.

Akiwa nchini Cameroon Katika ziara yake ya kwanza barani Afrika, Papa Benedict alisema matumizi ya kondom sio suluhisho la vita dhidi ya ukimwi. Bara la Afrika ndilo limeathirika pakubwa na ugonjwa wa ukimwi.


Mwaka wa 2009 ningetaka uwe mwaka wa Afrika....ndio yalikuwa matamshi ya kiongozi huyu wa kanisa la kikatoliki duniani....kabla hata hajakanyaga mchanga wa Afrika. Lakini alipowasili tu mjini Younde, awamu yake ya kwanza ya ziara ya wiki moja barani Afrika, Papa Benedict alifungua mlango wa mjadala mkali.


Usambazaji na matumizi ya kondom na mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi. Papa alisema mipira ya kondom sio suluhisho la kuzuia maambukizi na kusambaa kwa maradhi haya yanayowasononesha mamilioni ya raia barani Afrika.


'' Ukimwi sio janga linaloweza kutatuliwa na pesa pakee yake....ni janga haliwezi kukabiliwa na utumiaji wa mipira ya kondom...ambayo nadhani inachangia zaidi maambukizi.'' Ndio matamshi Papa aliyoyatoa punde tu alipowasili Younde.


Baba mtakatifu alisisitiza kuwa kujitolea kiroho, kuwaonyesha mapenzi wanaoishi na virusi vya ukimwi ni bora zaidi.


Lakini ni matamshi haya ndio yamezua utata, huku watalaam wa afya wakimkosoa Papa Benedict, wakisema ugonjwa wa ukimwi hauna uhusiano wowote na usambazaji wa mipira ya condom. Mtalaam mmoja wa afya anasema,

'' Hakuna ushahidi wowote unaonyesha kuwa usambazaji wa mipira ya kondom kwa watu wanaoutumia kondom kwa njia yeyote inawafanya wajihusishe na kufanya mapenzi yatakayohatarisha maisha yao.''


Wataalm huko Vatikani walinukuliwa wakisema hawajahi kumsikia Papa akitumia neno Kondom. Hii ndio ilikuwa mara ya kwanza.


Na katika mkutano na rais wa Cameroon Paul Biya, Papa pia aligusia swala lingine, ambalo limekita mizizi barani Afrika. Umasikini, migogoro ya kisiasa, ufisadi na njaa.

'' Pale raia wanapoteseka, kwa njaa, na umaskini mkubwa, katika vita vya wenyewe kwa wenyewe , ufisadi uliokithiri na matumizi mabaya ya mamlaka .....mkiristo yeyote hawezi kukaa kimya.'' Alisema baba mtakatifu.


Akimlaki Papa Benedict Afrika inaashiria watu wanaijali Afrika, bara linalotikiswa na magonjwa, umasiki na vita vya wenyewe kwa wenyewe. ndio yalikuwa matamshi ya Rais wa Cameroon Paul Biya alipomlaki mwenyeji wake.


Akiwa Yaounde Papa, pia atafanya mkutano na waakilishi wa mataifa 52. Huko Angola kiongozi huyu wa kanisa la kikatoliki atakutana na wanadiplomasia walioko Luanda, kusisitizia mataifa ya Magharibi yasilipe mgongo bara la Afrika. Ingawa hii ni ziara yake ya kwanza kama Papa barani Afrika, Benedict aliwahi kuzuru Afrika mwaka wa 1987 alipokuwa kadinali Joseph Ratzinger, wakati huo alifika katika nchi ya demokrasia ya Congo, wakati huo ikijulikana kama Zaire.MUNIRA MUHAMMAD/ AFP

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com