1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya makamu wa rais wa Marekani mashariki ya kati

Saumu Ramadhani Yusuf9 Machi 2010

Marekani yasema itaizuia Iran kutengeneza silaha za Nuklia kwa ajili ya kuilinda Israel

https://p.dw.com/p/MOBE
Makamu wa rais wa Marekani Joseph Biden,akipeana mikono na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu jumannePicha: AP

Makamu wa rais wa Marekani, Joe Biden, bado anaendelea na ziara yake katika eneo hilo. Nchini Israel ameuhakikishia utawala wa taifa hilo la kiyahudi kwamba  Marekani imejitolea kuutetea usalama wa taifa hilo, pamoja na  kuizuia Iran isitengeneze silaha za Kinyuklia. Aidha ameunga mkono suala la kufufuliwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina, chini ya upatanishi wa Marekani, akisema kwamba hiyo ndio nafasi ya wazi ya kufikiwa amani katika eneo hilo.

Makamu wa rais wa Marekani, Joe Biden, ambaye aliwasili Israeli jana Jumatatu amejadiliana masuala mengi pamoja na waziri mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, ikiwa ni pamoja na suala muhimu kwa Israeli la kuibinya Iran kuwekewa vikwazo juu ya mpango wake wa kinyuklia. Baada ya kuzungumza na waziri mkuu huyo wa Israel, Biden alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisisitiza juu ya msimamo wa Marekani kuelekea uhusiano wake na Israel na hasa katika suala la usalama, akisema-

''Hakuna pengo kati ya Marekani na Israeli linapokuja suala la usalama wa Israeli, na kutokana na sababu hiyo na nyinginezo kulishughulikia suala la Iran na mpango wake wa Kinuklia limekuwa ni jambo muhimu linaloangaliwa na utawala wa Marekani. Tumejitolea kuizuia Iran isitengeneze silaha za Kinuklia''

Joseph Biden Israelische Flaggen
Marekani yaihakikishia usalama Israel dhidi ya IranPicha: AP

Makamu huyo wa rais wa Marekani pia amefahamisha kwamba nchi yake inashirikiana na nchi nyingine katika jumuiya ya kimataifa kuishawishi serikali ya mjini Tehran kuzingatia masharti yaliyowekwa na  kusimamisha shughuli zake za kinyuklia. Kwa upande wake, waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye nchi yake inaaminika kuwa mmiliki pekee wa silaha za nyuklia  katika eneo hilo la Mashariki ya kati, ametaka Iran iwekewe vikwazo vikali zaidi vitakavyo hakikisha kwamba  biashara ya mafuta na gesi ya Iran imedhoofika kabisa.

''Tunamshukuru rais Obama kwa juhudi anazofanya kuiongoza jumuiya ya kimataifa kuiwekea vikwazo vikali Iran. Kwa kadri nchi hiyo itakavyowekewa vikwazo vikali ndivyo itakavyoweza kukaa chini na kuchagua kati ya kuendelea na mpango wake wa kiynuklia na hatima ya kuendelea kuweko kwake''

Ziara ya Biden imekuja wakati ambapo juhudi mpya za kutafuta amani kati ya Palestina na Israeli zimechacha, ambapo pande zote mbili zimekubaliana kukutana na mjumbe maalum wa Marekani katika eneo hilo, George Mitchell, wiki hii kwa ajili ya kufufua mazungumzo ya amani yaliyokwama tangu mwezi Desemba mwaka 2008. Sambamba na hayo, katika mkutano wake na makamu wa rais Joe Biden, waziri mkuu Benjamin Netanyahu amelizungumzia suala hilo la amani na Wapalestina, akisema kwamba yuko tayari kushirikiana na Marekani katika kufikia makubaliano ya amani na wapalestina-

Fatah Konferenz Mahmoud Abbas Flash-Galerie
Rais wa Palestina Mahmoud AbbasPicha: AP

''Nategemea kushirikiana na rais Obama pamoja na wewe na utawala mzima kufikia makubaliano ya amani ambayo yatazingatia uhalali wa taifa la kiyahudi la Irael litakalotambuliwa na majirani wa Palestina na ambayo yatazingatia usalama wa kizazi kijacho cha Israel''

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden atakutana pia na viongozi wa mamlaka ya wapalestina mjini Ramallah.

Mwandishi: Saumu Yusuf Ramadhan/ Reuters

Mhariri:  Miraji Othman