Ziara ya Gordon Brown Washington | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.07.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ziara ya Gordon Brown Washington

Waziri mkuu mpya wa Uingereza ameonana na George Bush,mshirika wa chanda na mpete wa mtangulizi wake Tony Blair.Je, siasa ya Uingereza kuelekea George Bush itabadilika ?

Kwa muda wa siku 2 ,waziri mkuu mpya wa Uingereza,Gordon Brown,amezuru Washington,mji mkuu wa Marekani na amemtembelea rais George Bush.Uingereza ndie mshirika wa chanda na pete wa Marekani barani Ulaya.Wakati huo huo lakini, visiwani Uingereza,shaka-shaka zimezidi juu ya siasa ya Marekani nchini Irak.

Katika ziara yake hii,hata waziri mkuu Gordon Brown aliempokea madaraka Tony Blair,rafiki wa chanda na pete wa George Bush alipaswa kuzingatia.

Kuwapakia katika kigari cha mchezo wa golf uwani Camp David na kumtembeza mgeni wake, ni heshima anayotoa Bush kwa wageni maalumu anaowatukuza.Madhumuni yake ni kubainisha usuhuba maalumu na kukinaiana.Hatahivyo, inadhihirika katika usuhuba kati ya London na Washington kuna kitu kilichobadilika.Na hii inatokana kuaga kwa Tony Blair maskani yake ya 10 Downing Street na ,kumpisha Gordon Brown.

Kwani, Blair na Bush walijenga usuhuba mkubwa na wa kuaminiana.Usuhuba uliobainika pale Marekani na uingereza bega kwa bega zilipoingia vitani nchini Irak.Hatua hii ilimharibia jina nyumbani waziri mkuu Blair na akionekana ni kikaragosi tu kinachochezeshwa na george Bush apendavyo.

Licha ya kuonesha jana hadharani kwamba Marekani na Uingereza hazikuingia ufa,Bw.Brown atachukua mkondo tofauti na mtangulizi wake Blair.

Ishara hizi zadhihirika pale Brown alipoamua kufanya ziara yake ya kwanza baada ya kumrithi uongozi Tony Blair haikuwa Washington bali Berlin.Isitoshe, George Bush yumo kufunga virago pole pole kun’gatuka madarakani na Brown hahitaji kupalilia usuhuba mwema na msala upitao.

Nani atakalia kiti cha Bush hapo baadae mwanamume au mwanamke,hataki Gordon Brown kuwa taabu kufanya kazi nae kurekebisha mambo nchini Irak.Na hii itakuwa kwake rahisi zaidi kuliko chini ya mkakamavu George Bush wakati huu.

Tayari vyombo vya habari vya Uingereza vinapiga upatu na kuhanikiza kwamba majeshi ya uingereza yakabidhi hatamu mikononi mwa vikosi vya Irak katika mji wa Basra,ambao kinyume na Baghdad,kuna hali ya utulivu kidogo.

Hata ili aweze kuchaguliwa tena katika uchaguzi ujao, Gordon Brown atakua na turufu kubwa zaidi ikiwa atajitenga mbali na george Bush.kwani kinyume na Bush,Brown inambidi kusimamia tena uchaguzi.

Ingawa waingereza wanaiangalia Marekani mshirika imara katika vita dhidi ya ugaidi ulimwenguni,lakini huko nchini hakuna mwanasiasa wa nje asiependeza machoni mwao kama George Bush.

Tangazo la hivi punde la Marekani kuziuzia nchi shirika za Mashariki ya kati silaha mpya,ni kero kwa Gordon Brown anaeweza kuhisi juhudi za mtangulizi wake Tony Blair alietwikwa jukumu la upatanishi huko Mashariki ya kati latiliwa kitumbua chake mchanga.

Chini ya hali hii,Gordon Brown itampasa kwenda na hali ya mambo ilivyo….

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com