1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky: Urusi yaendeleza mashambulizi mashariki ya Ukraine

Grace Kabogo
2 Februari 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ameelezea mashambulizi ya kutisha yanayofanywa na vikosi vya Urusi ambavyo vinasonga mbele kuelekea kwenye jimbo la mashariki la Donetsk na kuifanya hali kuwa ngumu zaidi.

https://p.dw.com/p/4N0Bq
Ukraine-Krieg | Folgen eines russischen Raketenangriffs in Kramatorsk
Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Katika tathmini ya kushangaza aliyoitoa usiku wa kuamkia Alhamisi wakati akilihutubia taifa, Zelensky amesema hali katika maeneo ya mapambano mashariki mwa Ukraine imekuwa mbaya huku vikosi vya Urusi vikizidi kusonga mbele, hatua inayoonesha kuwa vinaweza kufanya mashambulizi mapya Februari 24, wakati wa kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.

Zelensky amesema adui anajaribu kupata mafanikio ili kuonesha kuwa ana nafasi ya kufanya mashambulizi mapya wakati wa kumbukumbu hiyo. Jumatano usiku jeshi la Ukraine lilisema kuwa mji wa Bakhmut na jamii nyingine 10 zilishambuliwa Jumatano kwa makombora na vifaru vya Urusi.

Avdiivka na Maryinka pia yashambuliwa

Kwa mujibu wa jeshi hilo miji ya Avdiivka, Maryinka na baadhi ya maeneo ya makaazi pia yalishambuliwa. Urusi imedhamiria kusonga mbele kuelekea kaskazini na kusini mwa miji ya Bahkmut na Donetsk, kabla Ukraine haijapatiwa vifaru na magari ya kivita ilivyoahidiwa na mataifa ya Magharibi.

Wakati huo huo, Gavana wa jimbo la Donetsk Pavlo Kyrylenko amesema takribani watu watatu wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa katika shambulizi la roketi la Urusi lililotokea jana kwenye mji wa Kramatorsk katika jengo la makaazi ya watu. Akizungumzia vifo hivyo, Rais Zelensky amesema watu wasio na hatia wanakufa na wengine wamefunikwa kwenye vifusi. Amesema huo ndiyo ukweli wa maisha yao ya kila siku.

Ukraine Zusammenstöße zwischen Nationalisten und der Polizei in Kiew
2019, wanaharakati na wafuasi wa chama cha siasa cha National Corps walidai uchunguzi kuhusu ufisadi wa maafisa wa jeshi la Ukraine ufanyikePicha: Reuters/G. Garanich

Katika hatua nyingine Zelensky ameahidi kuongeza juhudi za kupambana na rushwa wakati ambapo maafisa wa Ukraine wanaendelea kuwasaka mafisadi, kabla ya mkutano wake na maafisa wa Umoja wa Ulaya uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa mjini Kiev, ikiwa ni katika kuonesha kuonesha dhamira yake kwamba inaweza kuaminiwa kutokana na msaada wa mabilioni ya dola ambao imekuwa ikipatiwa na kwamba watu hawatumii vibaya madaraka.

''Leo ofisi inayoshughulika na usalama wa uchumi imefanya misako kadhaa. Kwa bahati mbaya kwenye baadhi ya maeneo njia pekee ni kubadili uongozi. Mabadiliko kama haya ni muhimu kuhakikisha kwamba watu wanaheshimu utawala wa sheria,'' alifafanua Zelensky.

Marekani na Ujerumani na msimamo kuhusu ndege za kivita

Huku hayo yakijiri, kuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema hatoshangaa iwapo nchi kama vile Marekani na Ujerumani zitabadili msimamo wao wa kuipatia Ukraine ndege za kivita. Akizungumza na waandishi habari mjini Brussels, Borrell amesema hapo awali upelekaji wa vifaru Ukraine pia ulikuwa na utata mkubwa, lakini hatimaye makubaliano yalifikiwa. Amesema upelekaji wote wa silaha Ukraine hadi sasa umekuwa ukiambatana na kutolewa onyo kuhusu hatari inayowezakana ya kuongeza zaidi mzozo na Urusi.

Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki, alisema yuko tayari kupeleka ndege za kivita Ukraine. Hata hivyo, Mateusz amesema anaona hali ya kutoaminiana inaongezeka kwa Ujerumani. Amemkosoa Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz kwa kutomchukulia kwa umakini Rais wa Urusi, Vladmir Putin.

(DPA, AFP, AP, Reuters)