1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Zelensky akutana na viongozi wa Marekani, EU mjini Rome

18 Mei 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekutana na maafisa waandamizi wa Marekani na Ulaya mjini Rome. Ni kabla ya mazungumzo ya simu Jumatatu kati ya Marais wa Marekani na Urusi kuhusu kumaliza vita nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4uYPb
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika mkutano na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance
Zelensky alikutana mjini Rome na viongozi wa Marekani, EU mjini Rome kabla ya simu ya Trump na PutinPicha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout via REUTERS

Hiyo ni sehemu ya juhudi zilizoimarishwa za kidiplomasia kabla ya mazungumzo ya simu kesho Jumatatu kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi kuhusu kumaliza vita nchini Ukraine.

Zelensky alizungumza na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio katika makazi ya balozi wa Marekani. Kansela wa Ujerumani Friedriech Merz alisema alizungumza na Zelensky na Rubio pembezoni mwa misa ya kusimikwa rasmi kwa Papa Leo XIV iliyofanyika leo mjini Vatican.

Merz pia amesema amekubaliana na viongozi wa Ufaransa na Uingereza kuwa watazungumza tena na Rais wa Marekani katika maandalizi ya mazungumzo hayo ya simu. Merz amewaambia waandishi habari mjini Rome kuwa viongozi wa Ulaya na Marekani wamedhamiria kushirikiana kuhakikisha vita vinamalizika Ukraine.

Trump alisema anapanga kuzungumza na Putin na kisha Zelensky na viongozi wa nchi mbalimbali za Jumuiya ya NATO, kuhusu kumaliza vita hivyo.