1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zapatero ashinda uchaguzi nchini Hispania

M.Koch/P.Martin10 Machi 2008

Chama cha Kisoshalisti kinachotawala nchini Hispania kimeshinda uchaguzi wa Jumapili kwa wingi mkubwa zaidi ya vile ilivyotarajiwa kwa kujinyakulia asilimia 44 ya kura.

https://p.dw.com/p/DLhz
Spainish Prime Minister Jose Rodriguez Zapatero celebrates his party's, (PSOE) win, at the socialist party headquarters in Madrid, Sunday March 9, 2008. (AP Photo/Bernat Armangue)
Waziri Mkuu wa Hispania,Jose Rodriguez Zapatero afurahia ushindi wa chama chake cha Kisoshalisti(PSOE) mjini Madrid.Picha: AP

Licha ya chama cha kisoshalisti cha Waziri Mkuu Zapatero kujiimarisha bungeni,chama hicho hakitoweza kutawala peke yake,kwa hivyo kitapaswa kuunda serikali ya mseto pamoja na vyama vingine vidogo. Alipohotubia umati uliokusanyika mbele ya makao makuu ya chama chake cha Kisoshalisti Zapatero alisema,ataiongoza serikali yake kwa kufuatiliza mafanikio yaliyopatikana na kurekebisha makosa yaliyofanywa.Vile vile atakuwa na midahalo kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa.

Kwa upande mwingine,chama cha kihafidhina cha PP kinachoongozwa na Mariano Rajoy kimeshindwa kutimiza lengo lake kuingia madarakani.Baada ya kujinyakulia asilimia 40 ya kura chama hicho kitakuwa na viti 154 kulinganishwa na 169 vilivyoshindwa na chama cha kisoshalisti cha Zapatero katika bunge la wajumbe 350.Baada ya kushsindwa mara mbili kwa mfululizo,mustakabali wa Rajoy kama kiongozi wa chama cha PP unayumbayumba. Wakati huo huo ushsindi wa vyama viwili vikuu umeathiri vyama vidogo.Hata hivyo washirika wa chama cha Kisoshalisti kutoka majimbo ya Basque na Katalonia wamefanikiwa kungángánia viti vyao bungeni.Kwa hivyo,sasa si shida kwa serikali ya Zapatero kuwa na uwingi mkubwa bungeni. Akisisitiza hali hiyo mpya iliyoibuka,Zapatero amesema, wananchi wamedhihirisha kuwa wanataka enzi mpya isiyokuwa na mivutano wala mapambano.

Wakati wa utawala wake wa miaka minne,Zapatero amefanya mageuzi makubwa ya kijamii nchini Hispania. Miongoni mwa mageuzi hayo ni kuruhusa ndoa kati ya watu wa jinsia moja,kuharakisha utaratibu wa kutoa talaka pamoja na sheria za kuhimiza usawa wa kijinsia na kutoa msamaha wa jumla kwa wafanyakazi ambao hawakuwa na hati rasmi. Baadhi kubwa ya mageuzi hayo yamewahamakisha viongozi wa Kanisa la Katoliki lakini chama cha kihafidhina PP hakijatumia fursa hiyo kuzusha mdahalo kwa hofu kuwa hatua hiyo ingewafungamanisha wapiga kura wa mrengo wa shoto. Badala yake chama hicho cha upinzani kilitoa kipaumbele kwa masuala ya ukosefu wa ajira unaozidi kuongezeka na hofu kuhusu idadi kubwa ya wahamiaji wanaokimbilia nchi hiyo.

Rajoy aliewahi kuwa waziri wa elimu na waziri wa ndani ameiituhumu serikali ya Zapatero kuwa haina msimamo mkali kuhusu suala la ugaidi.Tuhuma hizo zilitolewa baada ya Zapatero kujaribu na kushindwa kufanikiwa katika majadiliano ya amani pamoja na kundi la ETA linalogombea uhuru wa jimbo la Basque.Zaidi ya watu 800 wameuawa katika kampeni ya ETA ya takriban miaka 40.Siku ya Ijumaa pia mbunge wa zamani wa chama cha kisoshalisti katika serikali ya mitaa Isaias Corrasco alipigwa risasi na kuuawa katika jimbo la kaskazini la Basque ikishukiwa kuwa ni magaidi wa ETA ndio waliohusika na mauaji hayo.