1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zanzibar: Mahakama Kuu yakataa maombi ya ACT Wazalendo

13 Februari 2026

Mahakama Kuu ya Zanzibar imeyatupilia mbali maombi madogo ya dharura, kuizuia Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) kuharibu nyaraka za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

https://p.dw.com/p/58jfM
Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi akiapishwa baada ya uchaguzi
Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi akiapishwa baada ya uchaguziPicha: Sudi Mnette/DW

Maombi hayo yaliyowasilishwa hivi karibuni na wagombea wa uwakilishi kutoka majimbo 17 ya Unguja na Pemba kupitia chama cha ACT Wazalendo  yaliyolenga kuizuia ZEC kuharibu nyaraka hizo, wakati wakiendelea na kesi za kupinga matokeo yaliyotangazwa kwenye uchaguzi huo wenye utata.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Salma Ali Hassan baada ya kukubaliana na hoja za walalamikiwa, ambao ni Tume ya Uchaguzi ZEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwamba hati za viapo za walalamikaji zilikuwa na kasoro za kiufundi.

Hata hivyo, tayari mwanasheria anayesimamia upande wawalamikaji, Wakili Omar Said Shaaban, tayari ameshafungua maombi upya Mahakama Kuu.

Mpiga kura akipiga kura yake Zanzibar
Mpiga kura akipiga kura yake ZanzibarPicha: Brian Inganga/AP Photo

Uamuzi huo unatokana na kesi ya msingi iliyofunguliwa wiki iliyopita, ambapo upande wa ACT Wazalendo uliiomba Mahakama Kuu kuiamuru ZEC kutokuendelea na uamuzi wa kuziteketeza nyaraka za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 katika kipindi hiki ambacho waliokuwa wagombea wake wanaendelea na kesi mahakamani kupinga matokeo yaliyotangazwa na ZEC kwenye uchaguzi huo.

ACT imekuwa ikiukosoa uamuzi wa ZEC

Mwezi uliopita, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji George Kazi, alisema wamechukuwa hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa kifungu 98[3] cha sheria ya uchaguzi kinachowapa ruhusa ya kuharibu nyaraka siku 90 baada ya uchaguzi kufanyika.

Lakini tangu hapo, chama cha ACT Wazalendo kimekuwa kikiukosowa uamuzi huo wa ZEC kikisema una nia ya kufuta ushahidi wa kesi zilizofunguliwa dhidi yake.

Wanachama wa chama cha ACT Wazalendo
Wanachama wa chama cha ACT WazalendoPicha: Office of the First Vice President of Zanzibar

Miongoni mwa nyaraka zilizotajwa kwenye maombi ya walalamikaji ni fomu mbalimbali zinazotumika wakati wa uchaguzi zikiwemo orodha za wapiga kura walioomba kushiriki kura ya mapema.

Kura ya mapema inayotambuliwa kupitia kifungu 81 cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Namba 1 ya mwaka 2018, hupigwa siku moja kabla ya kura inayoshirikisha watu wote.