1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZANU - PF kuamua hatma ya Mugabe

Zainab Aziz
19 Novemba 2017

kamati kuu ya chama kinachotawala nchini Zimbabwe cha ZANU PF watakutana leo hii kufanya maamuzi ya kumvua madaraka rais Robert Mugabe ambaye ameiongoza nchi hiyo tangu ilipopata uhuru wake miaka 37 iliyopita.

https://p.dw.com/p/2nsTI
Zimbabwe Präsident Robert Mugabe am Rednerpult bei der ZANU-PF
Picha: AP

Kwa mujibu wa wanachama wawili wa ZANU PF mkutano huo maalum wa wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho utaanza mwendo wa saa nne na nusu asubuhi. Ajenda kuu ni kuangalia uwezekano wa kumuondoa madarakani kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 ikiwa ni siku ya nne tangu jeshi la Zimbabwe lilipotwaa mamlaka, licha ya kusema halijafanya mapinduzi bali linapambana na wahalifu wanaomzunguka Rais Mugabe. Wakati huo huo, shirika la utangazaji la taifa nchini humo limetoa taarifa kwamba rais Mugabe atakutana na maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi. Shirika hilo limemnukuu padri mmoja wa kanisa Katoliki ambaye alikuwa ni msuluhishi katika mazungumzo na Rais Mugabe.

Maelfu ya watu waingia barabarani Harare

Simbabwe Proteste in Harare
Waandamanaji mjini HararePicha: picture-alliance/AP Photo/T. Mukwazhi

Wakati hayo yakiendelea, jana Jumamosi maelfu ya watu walimiminika barabarani katika mji mkuu wa Harare wakiimba na kucheza huku wakiwakumbatia wanajeshi, ishara kuwa wanaunga mkono hatua ya kumng'oa Rais Mugabe madarakani.

Simbabwe - Emmerson Mnangagwa
Emmerson MnangagwaPicha: Getty Images/A. Joe

Kamati kuu ya chama cha ZANU PF inatarajiwa kumrejeshea wadhfa wake wa makamu wa rais wa chama bwana Emmerson Mnangagwa. Hatua hiyo ni sawa na kuifufua amali ya kisiasa ya mkuu huyo wa zamani wa usalama ambaye alipewa jina la utani la "Crocodile”. Kuachishwa kwake umakamu wa rais siku chache zilizopita ndio sababu ya jeshi la Zimbabwe kuingilia kati.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, mke wa Rais Mugabe, Grace anatarajiwa kunyang'anywa mamlaka ya uongozi wa tawi la wanawake la chama cha ZANU PF. Hatua hiyo itakuwa ndio inagonga msumari wa mwisho katika kumuondoa kwenye medani za kisiasa mama huyo mwenye umri wa kiaka 52 ambaye wiki iliyopita alikuwa kwenye kilele cha kumrithi mumewe baada ya makamu wa rais bwana Mnangagwa kufukuzwa kazi.

Uungwaji mkono wadidimia

Robert Mugabe und Grace Mugabe
Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na mkewe Grace MugabePicha: Getty Images/J.Njikizana

Kuporomoka ghafla kwa Rais Mugabe na mkewe bila shaka kutakuwa ni ishara ya kuleta hofu katika bara la Afrika ambako viongozi wengi wasiotaka mabadiliko kama Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na mwenzake wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila wanaokabiliwa na shinikizo kwamba waachie madaraka. Rais Mugabe akiwa amezuiliwa nyumbani kwake amekataa katakata kuachia madaraka japo kuwa anaona wazi jinsi umaarufu wake ulivyo poromoka vibaya katika siku tatu kuanzia kwenye chama chake cha ZANU PF hadi kwenye vyombo vya usalama na wananchi kwa jumla.

Mugabe na mkewe Grace wasema bora wafe wakitetea haki

Simbabwe Mugabe Frauen protestieren gegen Menschenrechtsverletzungen
wanawake wa Zimbabwe washinikiza Mugabe aondokePicha: AP

Mpwa wa rais Mugabe Patrick Zhuwao ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Mzee Mugabe na mkewe wako tayari kufa wakitetea haki kuliko kung'atuka madarakani na kupisha kile wanachokiita mapinduzi.

Marekani ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikimkosoa Mugabe imesema inakaribisha mwanzo mpya wa Zimbabwe. Rais Ian Khama wa nchi jirani ya Botswana amesema Mugabe hakuungwa mkono kwenye ngazi za kidiplomasia katika kanda ya Afrika hivyo anastahili kujiuzulu. Katika barabara za mjini Harare ni wachache tu walioonekana kujali kuhusu sheria wengi wanasubiri kwa hamu "uhuru wa pili" wa nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa koloni la Uingereza wanazungumzia juu ya ndoto walizonazo za mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi baada ya miongo miwili ya ukandamizaji na shida.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE

Mahriri: Grace Patricia Kabogo