1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu milioni moja waandamana nchini Chile

Tatu Karema
26 Oktoba 2019

Zaidi ya watu milioni moja wameandamana nchini Chile katika maandamano makubwa zaidi ya kutaka mabadiliko ya kiuchumi na kujiuzulu kwa rais Sebastian Pinera.

https://p.dw.com/p/3Rz1B
Chile Proteste in Santiago
Picha: Reuters/I. Alvarado

Waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera za maeneo yao na ya kitaifa, waliimba nyimbo maarufu za ukaidi kutoka enzi ya uongozi wa kidikteta wa Augusto Pinochet wa mwaka 1973-90 huku taifa hilo ambalo kwa kawaida linaonekana kama thabiti zaidi katika Amerika ya Kusini, likikabiliana na ghasia mbaya zaidi katika muda wa miongo kadhaa.

Katika ukurasa wake wa twitter, gavana wa jimbo la Santiago Karla Rubilar aliitaja kuwa,'' siku ya kihistoria'' na kusifu,''maandamano ya amani.....yakiwakilisha ndoto ya Chile mpya.'' Rubilar amesema kuwa zaidi ya watu milioni moja walifanya maandamano kote nchini humo, huku baraza la mji wa Santiago likitaja idadi hiyo kuwa elfu 820 pamoja na idadi ya polisi.

Katika muda wa wiki iliyopita, ghadhabu ya raia wa Chile ilisambaa kama maandamano dhidi ya mfumo wa kijamii na kiuchumi ambao wengi wanahisi kuwa umewatenga huku wakipata mapato ya chini na mafao, gharama ya juu ya matibabu na elimu na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini.

Pinera aliandika katika mtandao wa twitter kuwa, '' Maandamano haya makubwa, ya furaha na amani leo, ambapo raia wa Chile  wametaka serikali ya haki na ya kujali wananchi, yanafungua fursa muhimu za siku za baadaye na matumaini.'' Aliongeza kuwa, '' Sote tumesikia ujumbe huo. Sote tumebadilika. Kwa umoja na usaidizi kutoka kwa Mungu, tutaendelea katika njia ya kuifanya Chile kuwa bora kwa wote.''

Mapema wiki hii, Pinera aliomba radhi kwa kushindwa kufikiri iwapo kunaweza kuzuka maandamano na kutangaza mikakati kadhaa iliyowekwa kuwafaidi watu kama vile kuongezwa kwa mafao ya kiwango cha chini na malipo ya ajira. Pia alitangaza mpango wa kutamatisha hali ya hatari ya serikali isiyokuwa ya kawaida na kuondoa marufu ya kutotoka nje usiku ijapokuwa hali hizo zinaendelea kwa siku ya saba sasa. Katika ghasia zilizozuka hapo awali, vituo vya mabasi viliharibiwa, maduka ya jumla kuchomwa na kuibiwa na barabara kadhaa kuwekewa vizuizi. Serikali ilipeleka maafisa elfu 20 wa polisi na wanajeshi mjini Santiago waliotumia gesi na mabomba ya maji kuwatawanya waandamanaji.

Maafisa wa usalama wamelaumiwa kwa kwa vifo 19 vya waandamanaji. Siku ya Alhamisi, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa unatuma kundi la maafisa wake kuchunguza madai hayo. Visa vibaya na vya kukamatwa kwa watu vimepungua katika siku zilizopita ikilinganishwa na mwanzoni mwa vugu vugu hilo. Waandamanaji walipokuwa wakipita nje ya ikulu ya rais, walimtusi Pinera na jeshi la nchi hiyo. Huku maandamano hayo yakionekana kuwa ya kupangwa, bado hayana viongozi wanaotambulika na yalichochewa zaidi kupitia mitandao ya kijamii.