1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 40 wauwawa Syria

10 Mei 2012

Kiasi ya watu 40 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 170 wamejeruhiwa vibaya nchini Syria baada ya kutokea miripuko miwili mikubwa katikati ya jiji la Damascus. Miripuko hiyo pia imeteketeza majengo na magari kadhaa.

https://p.dw.com/p/14sh6
In this photo released by the Syrian official news agency SANA, flames and smoke raise from burning cars after two bombs exploded, at Qazaz neighborhood in Damascus, Syria, on Thursday May 10, 2012. Two large explosions ripped through the Syrian capital Thursday, heavily damaging a military intelligence building and leaving blood and human remains in the streets. (Foto:SANA/AP/dapd)
Miripuko mjini DamascusPicha: AP

Miripuko hiyo imetokea majira ya saa moja na dakika 50 asubuhi ambapo kwa kawaida wafanyakazi kutoka maeneo tofauti ya jiji la Damascus wanawasili maofisini kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Shirikia la Uangalizi wa Haki za Binadamu nchini Syria, lenye makazi yake huko Uingereza, limesema idadi ya waliokufa inaweza kufikia 50, miongoni mwao wakiwemo raia na wanajeshi wa serikali.

Mwandishi mmoja wa habari, aliekuwepo karibu na eneo la tukio, alisema wahudumu wa hospitali wameonekana wakiikusanya miili ya binadamu baada ya miripuko hiyo, na kwamba magari na vyombo vingine vya usafiri vilivyokuwa karibu na eneo hilo vikiungua moto.

U.N. observers walk towards soldiers at a Syrian army checkpoint during a field visit in Douma city, near Damascus May 5, 2012, one of the locations where there are protests against the regime of Syrian President Bashar al-Assad. REUTERS/Khaled al-Hariri (SYRIA - Tags: POLITICS CIVIL UNREST MILITARY)
Walinzi wa amani wa UNPicha: Reuters

Ukuta wa Nje wa Jengo la Idara ya Upelelezi ya Jeshi umeporomoka, ingawa katika sehemu ya ndani ilionekana bado imara. Serikali ya Syria imetupa lawama kwa magaidi huku ikisema idadi kubwa ya watu wamepoteza maisha na kujeruhiwa.

Hata hivyo, upande wa upinzani nchini humo umedai kwamba serikali ndio iliyopanga tukio hilo. Afisa mmoja mwandamizi, Samir Nashar, amesema madhumuni ya shambulio hilo ni kuwasilisha ujumbe kwa waangalizi wa Umoja wa Mataifa waliopo nchini humo kwamba wako katika hatari na kuishawishi jumuiya ya kimataifa kwamba wanakabiliana na ugaidi, jambo ambalo si la kweli.

Mkuu wa mpango wa usuluhishi wa Umoja wa Mataifa, jenerali Robert Mood, ambae ameshuhudia balaa hilo, amesema huo ni ushahidi mwingine kuonesha wakati mgumu walionao wananchi wa Syria ,na hivyo kuitaka jamii ndani na nje ya taifa hilo kusadia kurejesha amani.

Kiusalama, jiji la Damascus lipo katika ulinzi na udhibiti mkali wa majeshi ya rais Bashar al-Assad pamoja na kukumbwa na mashambulizi kadhaa ya mabomu ambayo yamekuwa yakilenga vikosi vya jeshi au misafara ya wajumbe mbalimbali nchini humo.

Mripuko mwingine mkubwa kutokea Syria kwa hivi karibuni ilikuwa Aprili 27, pale ambapo mtu mmoja alipojitoa mhanga na kusababisha vifo vya watu tisa na wengine 26 kujeruhiwa.

Mgogoro wa Syria ulianza Machi 2011 pale ambapo umma ulipoamua kuingia mabarabarani kushinikiza mabadiliko ya kisiasa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinasema kwamba zaidi ya watu 9,000 wameuwawa tangu kuanza kwa machafuko nchini humo.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP/APE
Mhariri: Miraji Othman