1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 1,000 watiwa mbaroni Gabon

1 Septemba 2016

Zaidi ya watu 1000 wametiwa mbaroni na polisi nchini Gabon kufuatia vurugu za kupinga matokeo ya uchaguzi ambazo serikali inasema zimepangwa na upinzani kufuatia kuchaguliwa tena kwa Rais Ali Bongo katika uchaguzi.

https://p.dw.com/p/1JuPQ
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Nusu saa tu baada ya Ali Bongo kutangazwa mshindi wa uchagu..zi wa rais uliofanyika nchini humo mwishoni mwa juma wafuasi wa mpinzani wake mkuu Jean Ping walikabiliana na polisi, walipora maduka na kulitia moto eneo la bunge katika mji mkuu wa Brazaville.

Allain Claude Bilie msemaji wa serikali amesema Ping alikuwa akiutekeleza mpango huo wa kufanysa vurugu ambao ulikuwa umeandaliwa na kutangazwa kitambo.

Msemaji huyo wa serikali amesema Ping alikuwa ametamka kwamba asingelikubali matokeo hayo na kwamba angeliwataka wananchi watoke mitaani kuandamana kupinga matokeo hayo na hicho ndicho hasa alichokifanya.

Kuhesabiwa upya kura

Ping mwenye umri wa miaka 73 alijitangazia ushindi siku chache baada ya uchaguzi huo kwa kusema kwamba kura zilizohesabiwa kwa njia huru zimeonyesha kwamba alikuwa mshindi.

Jean Ping mgombea mkuu wa upinzani.
Jean Ping mgombea mkuu wa upinzani.Picha: Reuters

Ping ambaye sasa anataka kura zihesabiwe upya amesema "Kila mtu ndani na nje ya nchi anajuwa kwamba mimi ndio mshindi kwa uhakika kabisa hakuna shaka kwa hilo.Kile tunachotaka ni kuhesabiwa upya kwa kura kituo kwa kituo chini ya jumuiya ya kimataifa.Tafauti ya kura ni kubwa mno haiwezekani kabisa kwamba ameshinda."

Ping amesema hali ya upinzani kushinda imekuwa ikijirudia nchini humo kwa miaka 50 kwamba upinzani daima umekuwa ukishinda lakini katu haushiki madaraka.

Hata hivyo serikali imemtaka Ping ambaye hajulikani alipo awasilishe maombi rasmi ya kuhesabiwa huko upya kwa kura iwapo anahoji matokeo hayo.

Msemaji wa serikali amesema Gabon sio nchi ya udikteta na kwamba iwapo kuna mtu anataka kuhesabiwa upya kwa kura jambo hilo linaweza kufanyika kupitia mahakama ya katiba.

Watu 1,000 mbaroni

Kwa mujibu wa polisi watu zaidi ya 1000 wametiwa mbaroni nchini Gabon kati yao 600 hadi 800 wamekamatwa Brazaville na wengine katika miji mengine kwa kuhusika na vurugu hizo na uporaji ambao bado umekuwa ukiendelea kwenye vitongoji vya kimaskini.

Eneo la bunge likiwaka moto Brazaville.
Eneo la bunge likiwaka moto Brazaville.Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Wakati nchi hiyo ikielekea kwenye machafuko Ufaransa mkoloni wa zamani wa taifa hilo la Afrika ya Kati leo imeitaka serikali ya nchi hiyo kutowa ufafanuzi wa mahesabu ya kura ya kila kituo.

Jean-Marc Ayrault waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa amesema "Ufaransa ina wasi wasi na hali ya Gabon.Tungependa kura za wananchi ziheshimiwe na tunaamini kwamba ikibidi matokeo hayo yapingwe kupitia mchakato wa mahakama na sio kupitia ghasia.Na ili kutuma ujumbe madhubuti wa uwazi pia tungelitaka matokeo ya uchaguzi yaonyeshwe hadharani kwa kila kituo."

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amelaani ghasia hizo na uporaji zilizozuka baada ya uchaguzi nchini Gabon na amezitaka pande zote mbili kuchukuwa hatua za kuleta utulivu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP/dpa

Mhariri :Gakuba Daniel