1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya wahamiaji 600 waokolewa Bahari ya Mediterania

Angela Mdungu
12 Agosti 2023

Meli ya hisani ya Ocean Viking imewaokoa zaidi ya wahamiaji 600 waliokuwa kwenye boti ndogo katika bahari ya Mediterania. Ni katika operesheni 15 zilizofanywa ndani ya saa 48.

https://p.dw.com/p/4V5w0
Wahamiaji walio kwenye boti wakisubiri kuokolewa
Wahamiaji walio kwenye boti wakisubiri kuokolewaPicha: Darrin Zammit Lupi/REUTERS

Kulingana na shirika la SOS Méditerranée, linaloendesha meli hiyo, operesheni nyingi za uokoaji zilifanyika kati ya mji wa bandari wa Sfax nchini Tunisia na kisiwa cha Lampedusa cha Italia. Shirika hilo la barani Ulaya lilichapisha taarifa za uokoaji Ijumaa jioni kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X ambao awali ulijulikana kama Twitter na kuongeza kuwa, harakati za uokoaji ziliratibiwa na mamlaka za Italia.

Shirika la SOS limesema kati ya wahamiaji 623 waliookolewa, 15 kati yao ni watoto na 146 ni watoto wengine ambao hawakuwa na wazazi, ndugu wala walezi walioambatana nao.

Soma zaidi: Je, wasafirishaji haramu wa binadamu ni akina nani?

Wahamiaji hao ni raia wa Sudan, Guinea, Burkina Faso, Ivory Coast, Benin na Bangladesh. Kwa mujibu wa SOS, wahamiaji waliookolewa wako salama na walikuwa wakipatiwa huduma ndani ya meli ya Ocean Viking.

Baadhi yao walitarajiwa kupelekwa katika pwani ya Lampedusa na wengine katika mji wa Civitaveccia, kaskazini magharibi mwa Roma.

Wahamiaji wengine 6 wamekufa kwa ajali ya boti Ufaransa

Katika mkasa mwingine uliotokea Jumamosi asubuhi, wahamiaji 6 wamefariki dunia na wengine wasiopungua 50 wameokolewa baada ya boti iliyokuwa inauvuka mlango bahari kutoka Ufaransa kwenda Uingereza kupinduka.

Msemaji wa mamlaka uagalizi wa pwani ya Ufaransa, Premar, amesema wahamiaji wengine kati ya watano hadi 10 hawajulikani walipo. Meli nne za Ufaransa, mbili za Uingereza na helikopta zilikuwa katika zoezi la uokoaji nje kidogo mwa Sangatte kaskazini mwa Ufaransa ilikotokea ajali hiyo. Meli za Uingereza ndizo zilizofanikiwa kuwaokoa wahamiaji waliosalimika.

Soma zaidi: Zaidi ya wahamiaji 100,000 wavuka ujia wa maji wa Uingereza

Tarifa ya mwanzo iliyotolewa na maafisa wa Ufaransa ilisema kuwa, mhamiaji mmoja mwenye asili ya Afghanistan alikufa kwenye ajali hiyo na kuwa wengine watano walikuwa katika hali mbaya. Awali Meya wa eneo hilo Franck Dhersin alisema kuwa, operesheni za uokoaji zilianza tangu saa kumi na mbili asubuhi wakati boti zaidi ya kumi zilipokuwa zikijaribu pia kuvuka mlango bahari huo wakati huo huo.

Mlango Bahari kati ya Ufaransa na Uingereza, ni moja kati ya maeneo yenye shughuli nyingi zaidi za usafirishaji na mawimbi yake ni yana nguvu kubwa. Idadi ya wahamiaji wanaowalipa walanguzi wa binadamu ili kufanya safari hatari za kuvuka bahari kwenda Ulaya, inazidi kukua kila mwaka. Mamia ya watu huzama kila mwaka wakazi boti zao zinapozama au kupinduka.