Zaidi ya waandishi wa habari 100 wauawa 2013 | Masuala ya Jamii | DW | 31.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Zaidi ya waandishi wa habari 100 wauawa 2013

Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari-IFJ, leo (31.12.2013) limetoa ripoti yake ya mwaka huu wa 2013, likionyesha idadi ya waandishi wa habari waliouawa wakiwa kazini katika maeneo mbalimbali duniani.

Waandishi wa habari wa Misri wakiwa katika mgomo mjini Cairo

Waandishi wa habari wa Misri wakiwa katika mgomo mjini Cairo

Kwa mujibu wa Shirikisho hilo kiasi waandishi wa habari 108 wameuawa kwa mwaka huu, huku waandishi wengi wakiwa wameuawa kutokana na mzozo wa Syria na kufuatiwa na mauaji ya Iraq.

Idadi hiyo imepungua kwa asilimia 10 ikilinganishwa na waandishi wa habari waliouawa mwaka uliopita wa 2012, lakini Shirikisho hilo la kimataifa la waandishi habari mesema serikali zinahitaji kuongeza juhudi za kumaliza mauaji hayo.

Ripoti hiyo ya IFJ iliyotolewa leo Jumanne (31.12.2013), imeeleza kuwa viwango vya mizozo bado havikubaliki na kuna haja ya haraka kwa serikali kuwalinda waandishi wa habari pamoja na kutekeleza haki zao za msingi.

IFJ yatoa wito kwa serikali

Shirikisho hilo limetoa wito kwa serikali ulimwenguni kote kukomesha uonevu na unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wote wa kwenye vyombo vya habari. IFJ imeiorodhesha Syria kama nchi hatari zaidi ambapo waandishi wa habari 15 wameuawa nchini humo, ikifuatiwa na Iraq ambako waandishi wa habari 13 waliuawa.

Nchi nyingine zinazofuatia ni Pakistan, Ufilipino na India ambako waandishi 10 waliuawa, Somalia wameuawa waandishi saba na waandishi wa habari sita wameuawa nchini Misri.

Shirikisho hilo ambalo linawawakilisha zaidi ya waandishi wa habari 600,000 katika nchi 134 duniani, limesema kuwa waandishi wa habari wa kike wamekuwa wakikabiliwa zaidi na kuongezeka kwa ghasia.

Katibu Mkuu wa IFJ, Eden White

Katibu Mkuu wa IFJ, Eden White

Waandishi wa habari sita wameuawa mwaka huu wa 2013 na wengine wengi wamekuwa waathirika wa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na vitisho.

Ripoti za mashirika mengine ya vyombo vya habari

Mwanzoni mwa mwezi huu, shirika la kimataifa la kutetea haki za vyombo vya habari linalojulikana kama "Waandishi wa Habari wasio na mipaka", lilisema kuwa waandishi wa habari 71 waliuawa kwa mwaka huu, lakini utekaji nyara uliongezeka kwa kasi.

Nayo Taasisi ya Kimataifa ya Waandishi wa Habari-IPI, yenye makao yake mjini Vienna, imesema waandishi wa habari waliouawa kwa mwaka huu hadi sasa ni 117 na kuufanya mwaka huu wa 2013 kuwa mwaka wa pili mbaya zaidi tangu ianze kurekodi mauaji ya waandishi wa habari duniani mwaka 1997.

Kwa mujibu wa IPI, mwaka 2012 ulikuwa mbaya zaidi ambapo waandishi wa habari 132 waliuawa, huku 39 wakiwa wameuawa nchini Syria.

Ama kwa upande wake Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari-CPJ yenye makao yake mjini New York imesema waandishi wa habari waliouawa kwa mwaka huu ni 70, wakiwemo wanane waliouawa mwezi huu wa Desemba.

CPJ imesema Syria ndiyo inaongoza kwa vifo hivyo, ambapo waandishi wa habari 28 waliuawa. Utafiti wa Shirikisho hilo la Kimataifa la Waandishi wa Habari-IFJ, uliwahusisha wafanyakazi wa vyombo vya habari kama vile wapiga picha na watangazaji.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com