1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya 100 wahofiwa kufa kwa maporomoko ya ardhi China

25 Juni 2017

Takriban miili 15 imepatikana huku zaidi ya watu 100 wakiwa bado hawajulikani walipo ikiwa ni masaa kadhaa baada ya maporomoko makubwa ya ardhi yaliyofukia kijiji cha Xinmo Kusinimagharibi mwa China Jumamosi (24.06.2017)

https://p.dw.com/p/2fKW9
China | Erdrutsch in China verschüttet Dorf
Picha: Reuters/China Stringer Network

Takriban miili 15 imepatikana huku zaidi ya watu 100 wakiwa bado hawajulikani walipo ikiwa ni masaa kadhaa baada ya maporomoko makubwa ya ardhi yaliyofukia kijiji cha Xinmo Kusinimagharibi mwa China wakati kiza cha usiku kikianza kuingia Jumamosi(24.06.2017)

Timu ya uokozi iliwatoa manusura hao baada ya kuchimba kwenye majabali yaliyowafukia.Familia moja tu na mtoto wao mchanga waliokolewa na kukimbizwa hospitali baada ya nyumba 62 za kijiji hicho kufukiwa na majabali na udongo baada ya upande mmoja wa mlima kuanguka katika jimbo la Sichuan.

Serikali ya kaunti ya Mao  ilisema hapo awali kupitia mtandao wa kijamii wa Weibo kwamba miili sita  ilipatikana, huku mingine kama 112 ikiwa bado haijulikani mahali ilipo. Shirika la habari la serikali nchini China mapema liliarifu zaidi ya watu 120 hawajulikani walipo.

Kwa mujibu wa shirika hilo la habari la taifa maporomoko hayo ya matope na majabali yameziba mto wenye urefu wa maili moja na barabara ya kilomita 1.6. Wakati usiku ukiingia mafisa wa serikali walitumia kandili kuleta mwanga kwenye vifusi wakati wafanyakazi wa uokozi wakiwa wamevaa koficha za chuma zenye kutowa mwanga unaowasaidia kupekuwa kwenye majabali wakisaidiwa na mbwa wenye kutafuta kwa kutumia harufu.

Hakuna dalili ya kijiji

China | Erdrutsch in China verschüttet Dorf
Juhudi za uokozi zikiendelea.Picha: Reuters/China Stringer Network

Takriban polisi 2,000,wanajeshi na raia wanashiriki katika shughuli hizo za uokozi wengine wakitumia mikono yao mitupu.Matinga tinga na magari ya kuchimba ambayo yalikuwa yakitumika wakati wa mchana yamesita kufanya kazi wakati kiza kilipoingia kutokana na mwangaza kuwa mbaya.

Picha zilizochukuliwa kutoka angani hazionyeshi dalili ya kuwepo kijiji hayo yanatajwa kuwa ni maporomoko ya ardhi ya maafa makubwa kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo tokea tetemeko la ardhi la Wenchuan ambalo liliuwa watu 87,000 hapo mwaka 2008 katika mji wa Sichuan.

Maporomoko ya ardhi ni hatari inayotokea mara kwa mara katika maeneo ya vijijini na milimani nchini China hususan wakati wa mvua kubwa. Mojawapo ya maporomoko yaliosababisha maafa makubwa yalitokea mwaka 1991 ambapo watu 216 walikufa katika jimbo la kusini magharibi la Yunnan.

Mwandishi : Mohamed Dahman

Mhariri : Lilian Mtono