Yemen,kambi ya magaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Yemen,kambi ya magaidi

Hadi siku za hivi karibuni Yemen ilikuwa nchi ya kuvutia sana kwa watalii kutoka nchi za magharibi.Lakini siku hizo zimeshapita. Hali ya usalama imebadilika.Yemen imegeuka kambi ya mafunzo kwa magaidi.

Yemen katika mgogoro

Yemen katika mgogoro

Raia wa nchi za nje waliondoka Yemen siku nyingi. Watu kutoka nchi za magharibi wanaokwenda Yemen ni wale walioingia katika uislamu au wanafunyzi wa Koran na chipukizi wa ugaidi. Yemen sasa imegeuka mahala pa mapunziko kwa waislamu wenye itikadi kali. Idara ya ujasusi ya Marekani inaamini kwamba tawi la al-Qaeda nchini Yemen ndilo linalofanya kazi kwa bidii kubwa kabisa katika eneo la Arabuni.

Mabomu ya vifurushi vilitokea Yemen mwishoni mwa mwaka wa 2010.Mabomu hayo yaligunduliwa ndani ya ndege kadhaa. Omar Faruk Abdulmutallab -gaidi kutoka Nigeria pia alijibanza nchini Yemen kabla ya kujaribu kujiripua ndani ya ndege iliyokuwa angani kuelekea Marekani mnamo mwaka 2009.

Mtaalamu wa masuala ya siasa na ya Mashariki ya kati Peter Pawelka amesema Yemena haina serikali kuu yenye nguvu; hali hiyo imekuwa kama sumaku inayowavuta magaidi wa al-Qaeda. Magaidi hao wanaweza kujipatia uwanja wa kutosha ambapo wanaendesha mafunzo ya kiitikadi na yamapigano.

Waziri wa ulinzi wa Yemen Mohammed Nasser Ali amesema kuwa jeshi la nchi yake halina uwezo wa kuwashinda wapiganaji wa al-Qaeda .Waziri huyo amesema ili kuweza kupambana na al-Qaeda nchi yake inahitaji kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa.

Tokea Rais mpya Abd Rabbo Mansur Hadi aingie madarakani makundi yenye itikadi kali ya kiislamu yameshawaua wanajeshi wa Yemen 250. Alipoingia madarakani Rais Mansur Hadi aliahidi kuchukua hatua kali dhidi ya al-Kaida. Lakini badala yake mashambulio ya magaidi hao yanaongezeka nchini Yemen.

Mtandao wa al-Qaeda pia umelianzisha kundi jingine nchini humo katika miezi ya hivi karibuni, linaloitwa Ansar al -Sharia yaani wafuasi wa sharia ya kiislamu.

Mtaalamu wa masuala ya ugaidi nchini Yemen Nabil Bukari amelifananisha kundi hilo na Taliban. Tofauti na al-Qaeda kundi la Ansar al -Sharia halina makusudi ya kufanya mashambulio ya kigaidi katika nchi za magharibi. Kiitikadi hakuna tofauti baina ya kundi hilo na mtandao wa al-Qaeda lakini lengo lake siyo kuendesha harakati za jihadi duniani kote, bali kuunda nchi huru.

Magaidi wameshafanikiwa kujenga ngazi ya kwanza katika hilo nchini Yemen.Wakati maandamano ya kuipinga serikali yalipofikia kilele mwezi machi mwaka jana katika miji ya Sanaa na miji mingine,magaidi waliitumia hali hiyo na kuuvamia mji wa Jaar.Muda mfupi baadae waliuchukua mji wa Zinjibar.Sasa wapiganaji wa kundi la Ansar al Sharia wanakusanya kodi katika miji wanayoidhibiti.

Wapiganaji hao wameandaa mipango ya kutoa huduma ya umeme na pia wameanzisha mahakama za kiislamu. Wachunguzi wamesema miji inayodhibitiwa na wapiganaji hao ni nakala ndogo za utawala wa Taliban.Marekani tayari imeshachukua hatua dhidi ya wapiganaji hao. Imeimarisha mashambulio ya makombora na ya ndege zake zisizokuwa na rubani.

Mwandishi:Naumann Nils

Tafsiri:Mtullya Abdu

Mhariri:Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com