1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yemen imepuuzwa - Umoja wa Mataifa

18 Mei 2016

Mkurugenzi wa Operesheni za Kibinadamu za Umoja wa Mataifa, John Ging, anasema ni 16% tu ya fedha za msaada kwa Yemen zilizokwishapatikana hadi sasa, akionya kuwa raia milioni 7.6 wanakabiliwa na janga la njaa.

https://p.dw.com/p/1Ipdf
Rai ya msaada kwa yemeni yaitikiwa kwa asilimia 16 tu
Mkurugenzi Huduma za Msaada, UN-John GingPicha: picture-alliance/AA

Kauli ya Ging inafuatia safari aliyoifanya nchini Yemen kutathmini hali ya kibinadamu, ambayo amesema imezidi kuzorota. Akizungumza na waandishi wa habari baadaye, kiongozi huyo amesema mzozo wa kibinadamu nchini Yemen hauzingatiwi kwa uzito unaostahili.

''Kupuuzwa huko kunadhihirika uitikiaji mdogo sana wa kutoa misaada'', amesema Ging, na kuongeza kuwa mpango wa msaada wa kibinadamu kwa Yemen umetekelezwa kwa asilimia 16 tu. ''Tulikuwa tumeomba dola za kimarekani bilioni 1.8, kiwango ambacho pia kinaonyesha ukubwa matatizo yanayowakumba watu huko.'' amesema afisa huyo.

Mkurugenzi huyo wa operesheni za kibinadamu amazisihi serikali ambazo zimepokea maombi mengi ya msaada kutoisahau Yemen, akizitaja Marekani, Uingereza, Kamisheni ya Umoja wa Ulaya na Japan, kuwa tayari zimekwishatoa michango kwa ajili ya Yemen mwaka huu wa 2016.

Pengo la Saudi Arabia ladhihirika

Tofauti kubwa na mwaka jana, amesema Ging, ni kukosekana kwa mchango wa Saudi Arabia mwaka huu. Nchi hiyo ambayo inaongoza operesheni ya anga dhidi ya waasi wanaoipinga serikali ya Yemen, mwaka jana ilikuwa imechangia dola milioni 245 katika mfuko wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Yemen.

Idadi kubwa ya wayemen wamekimbilia nje ya nchi yao.
Idadi kubwa ya wayemen wamekimbilia nje ya nchi yao.Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/A. Al Share

John Gings amezitaka nchi nyingi zaidi kuchangia katika mfuko huo, hususan akizitaja nchi za ghuba ya Uarabu, akisisitiza michango yoyote kutoka nchi zinazohusika katika mzozo wa Yemen haipaswi kuandamana na masharti yoyote.

Umoja wa Mataifa utaitisha mkutano kuhusu msaada wa kibinadamu mjini Istanbul, Uturuki, na mada kuu itakuwa uchangiaji wa fedha kugharimia msaada huo. Imedhihirika kuwa maombi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya msaada wa aina hiyo hayaitikiwi kwa zaidi ya asilimia 50, na kwa hivyo lazima njia nyingine ipatikane ya kuukusanya.

Hali ya kibinadamu imezorota

Ging amesema wayemen zaidi ya milioni 10 wanahitaji huduma za msingi za afya, huku mamilioni wengine wakikabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula na lishe bora. Aidha, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema watu 6,000 wamekwishauawa katika mzozo wa Yemen, wakiwemo watoto 930.

Yemen inakabiliwa na vita vikali baina ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao unaiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa, na waasi wa kihouthi ambao ni wa madhehebu ya kishia, wanaoudhibiti mji mkuu, Sanaa tangu Septemba 2014.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Yemen Abdul Malik al-Mekhlafi alitangaza jana kujiondoa katika mazungumzo ya amani yanayofanyika nchini Kuwait, baada ya wiki kadhaa za mkwamo. Waziri huyo ameushutumu upande wa wahouthi kukataa uhalali wa serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, rtre

Mhariri: Caro Robi