Yanayoweza kutokea baada ya uchaguzi wa Zimbabwe | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Yanayoweza kutokea baada ya uchaguzi wa Zimbabwe

Wachamuzi wanasema Mugabe yuko imara

Rais Robert Mugabe akiwa na wafuasi wake

Rais Robert Mugabe akiwa na wafuasi wake

Leo ni leo msema kesho ni muongo. Uchaguzi wa Zimbabwe unafanyika na mshindi atajulikana wakati vituo vya kupigia kura vitakapofungwa leo jioni. Je, ni mambo gani lakini yanayoweza kutokea nchini Zimbabwe iwapo rais Mugabe atashinda uchaguzi wa leo?

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, anakabiliwa na changamoto kubwa katika kipindi cha miaka 28 ya utawala wake huku uchaguzi mkuu wa rais, bunge na uchaguzi wa serikali za mitaa ukifanyika leo nchini humo.

Huku Zimbabwe iliyokuwa zamani imeendelea kiuchumi, ikikabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, Mugabe mwenye umri wa miaka 84 anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa waziri wake wa fedha wa zamani, bwana Simba Makoni, na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change, MDC, Morgan Tsavingari. Bila shaka matokeo yatakuwa na athari mbalimbali kulingana na nani atakayeshinda uchaguzi huo.

Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema iwapo rais Mugabe atashinda kwa asilimia 51 ya kura, atakwepa awamu ya pili ya uchaguzi. Mugabe anatarajiwa na wengi kushinda uchaguzi wa leo akiwategemea sana wafuasi wa chama chake cha ZANU-PF walio katika ngome zake za mashinani. Lakini baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanaamini rais Mugabe atatumia mamlaka yake kubadili matokoe ya uchaguzi huo.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change, Morgan Tsvangirai, huenda akayakataa matokeo ya uchaguzi kwa madai ya kuwepo na mizengwe na wafuasi wake huenda wakajitokeza mabarabarani kufanya maandamano. Hata hivyo hakuna uwezekano wa hali kama ile iliyojitokeza nchini Kenya ya maandamano ya muda mrefu na umwagaji damu kutokea nchini Zimbabwe.

Simbabwe, Morgan Tsvangirai, Oppositionsführer

Kiongozi wa wa chama cha MDC Morgan Tsvangirai

Serikali itawapeleka maafisa wengi wa polisi wa kupambana na ghasia kuwatandika bila huruma waandamanaji na huenda ikatishia kuwatia mbaroni na kutangaza utawala wa hali ya hatari. Wachambuzi wengi watatazamia maandamano kumalizika kwa haraka. Rais Mugabe huenda akaanzisha operesheni ya kuwasafisha wafuasi wa mpinzani wake Simba Makoni ndani ya chama cha ZANU-PF na serikalini.

Ikiwa rais Mugabe atashinda idadi kubwa ya kura lakini ashindwe kupata asilimia 51 ya kura inayotakikana kuwa mshindi wa moja kwa moja, atalazimika kuingia katika awamu ya pili ya uchaguzi. Inakisiwa atashindana na Tsvangirai katika awamu hiyo. Kampeni ya Makoni imesema itamuunga mkono kiongozi wa upinzani iwapo jambo hili litatokea.

Kukiwa na awamu ya pili, rais Mugabe atatarajiwa kuwatuma wapiganaji wa ZANU-PF katika maeneo yote ya Zimbabwe pamoja na wapiganaji wa zamani wa kivita waliopigania uhuru ili kuwashawishi wapigaji kura wampigie kura Mugabe. Hali hii inazusha uwezekano wa kufanyika machafuko kati yao na wafuasi sugu wa chama cha upinzani cha MDC katika kipindi cha majuma matatu kabla awamu ya pili ya uchaguzi kufanyika.

Awamu ya pili huenda imalizikie na Mugabe akitangazwa kuwa mshindi, hivyo kuacha hali ya wasiwasi wa kisiasa na pasipo na matumaini ya kuuokoa uchumi wa Zimbabwe ambao tayari umesambaratika. Nchi za magharibi huenda ziongeze vikwazo dhidi ya serikali ya Mugabe na kiongozi huyo huenda mamlaka yake yakadhoofika ndani ya chama chake cha ZANU-PF.

Simbabwe Wahlen Simba Makoni

Simba Makoni

Morgan Tsvangirai na Simba Makoni wote wakidai wameshinda uchaguzi, wafuasi wao wataanza maandamano ya barabarani kumlazimisha rais Mugabe akubali kushindwa. Serikali itawashutumu viongozi wa upinzani kwa makosa ya uhaini na kwa kujaribu kupindua utawala wa sheria.

Lakini upinzani utaunda muungano kushinikiza suluhisho lipatikane, hivyo kuyapa msukumo mpya maandamano ya barabarani na kuzusha ukosoaji mkubwa katika ngazi ya kimataifa dhidi ya rais Mugabe.

Ikiwa Simba Makoni, anayeungwa mkono ndani ya chama tawala cha ZANU-PF na wapinzani, atashinda, na jeshi na vyombo vya usalama vimkubali kama kiongozi anayeweza kuiunganisha Zimbabwe, rais Mugabe huenda akubali kushindwa.

Iwapo Morgan Tsvangirai atashinda lakini chama cha ZANU-PF na vyombo vya usalama vimkatae, kutatokea ukandamizaji mkubwa dhidi ya chama anachokiongoza cha MDC. Hili lakini linaonekana kuwa jambo ambalo kwa kiwango kidogo linaweza kutokea, hususan ikizingatiwa kwamba rais Mugabe ameudhibiti kwa mkono wa chuma mfumo unaosimamia uchaguzi nchini Zimbabwe na anaungwa mkono na vyombo vya usalama.

 • Tarehe 28.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DWh2
 • Tarehe 28.03.2008
 • Mwandishi Charo, Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DWh2
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com