1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaliyozingatiwa na wahariri ya magazeti leo hii

Dreyer, Maja1 Aprili 2008

Masuala yanayozungumziwa leo na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii ni Iraq, Zimbabwe na michezo ya Olimpiki.

https://p.dw.com/p/DYfT
Wanamgambo wa jeshi la Mahdi wa IraqPicha: AP


Suala moja ambalo linashughulikiwa kwenye kurasa na wahariri mara kwa mara ni Iraq. Tusikie basi kwanza maoni ya mhariri wa gazeti la "Financial Times Deutschland" kuhusu matukio ya Iraq ya hivi karibuni:


"Waziri mkuu Nuri al Maliki alitumia maneno makali pale aliposema kwamba hakutakuwa na mazungumzo na makubaliano wakati jeshi lake lilipoanza na operesheni yake dhidi ya wanangambo wa Kishia mjini Basra. Lakini inaonekana kama hata hivyo kulifanywa mazungumzo kwa vile kiongozi wa wanangambo Mahdi, Muktada al Sadr aliwaambia wafuasi wake kuweka chini silaha zao na kuitikia serikali. Haijulikani Iran ina jukumu gani kama mpatanishi katika mazungumzo hayo. Lakini itajaribu kuweka usawa kati ya makundi yanayopigana Iraq kwani si Irak yenye nguvu wala yenye machafuko yenye manufaa na nchi jirani ya Iran."


Ni uchambuzi wa gazeti la "Financial Time Deutschland" juu ya hali nchini Iraq na mahusiano na Iran. Tuelekee Zimbabwe sasa ambako bado matokeo ya mwisho ya uchaguzi hayakupatikana hadi sasa. Mhariri wa "Badisches Tagblatt" lakini tayari ametoa uamuzi wake. Ameandika:


"Kisa cha Robert Mugabe ni sawa na kile cha viongozi wengi duniani: Wamefanya vitu vingi vizuri lakini hawataki kuacha maradaka na hatimaye wanageukia kuwa wadhalimu. Ardhi ya wazungu Mugabe hajawapa wakulima maskini bali kwanza aliwanufaisha wenzake matajiri na wafuasi wake ambao walipigana pamoja naye katika vita vya ukombozi. Lazima achukue dhamana kwa makosa yake na kuirudishia jamii ya Zimbabwe yale alichoiibia."


Na mada yetu ya tatu na ya mwisho ni michezo ya Olimpiki itakayofanyika China mwaka huu na ambayo inaendelea kuzusha wasiwasi. Kama ni desturi ya michezo hii, mwenge wake utasafirishwa duniani kote hadi kurudi China kabla ya michezo kuanza. Safari hii ya mwenge inaitwa "Safari ya amani" lakini wengi wanajiuliza amani iko wapi? Hayo ni maoni ya gazeti la "Abendzeitung" la mjini Munich:


"Mwanzo wa safari hiyo ya amani ulikuwa kwenye uwanja wa Tian'anmen ambako mwaka 1989 maandamano ya kupigania demokrasia yalivunjwa kwa nguvu. Amani na Uhuru ni maneno ambayo hayaendi sambamba na namna polisi na jeshi la China liliulinda vikali uwanja huu. Wageni walioruhusiwa kuhudhuria sherehe walichaguliwa vizuri, waandishi wa habari walizuiliwa kufanya kazi zao. Basi, je, kweli kuna watu ambao wanaamini hali hii itaboreka? Kweli, michezo hii itakuwa ya furaha na bila siasa? Lengo la China ni kwamba michezo mizuri ya Olimpiki ifiche sura mbaya ya nchi hii. Lakini hata mamia ya medali za dhahabu hayawezi kuficha ukandamizaji na matumizi ya nguvu."