Yaliyoandikwa na wahariri wa Ujerumani hii leo | Magazetini | DW | 02.08.2005
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Yaliyoandikwa na wahariri wa Ujerumani hii leo

Hali nchini Saud Arabia baada ya kufariki dunia mfalme Fahd,kuteuliwa John Bolton kua balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa na mgomo wa madaktari nchini Ujerumani ndizo mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Hali nchini Saud Arabia imechambuliwa na gazeti la MANNHEIMER MORGEN linalosema:

„Sifa njema ya wasuudia imetuwama katika utilivu na utajiri.Hali lakini si tulivu hivyo tukitilia maanani mashambulio ya kigaidi yaliyoitikisa nchi hiyo.Na Utajiri nao pia unawekewa suala la kuuliza.Maisha ya raha na anasa waliyokua nayo familia ya Fahd ,yamekwisha ,na hata ukoo wa kifalme haumwagi tena fedha za mafuta ya petroli ovyo ovyo kama walivyokua wakifanya hapo zamani . Kwa vyovyote vile lakini hali yao bado ni ya mastarehe ikilinganishwa na ile ya wanaowatawala.Umaskini si neno geni tena nchini humo.Na mafuta,ambayo kila mmoja anayategea,yanazidi kupunguwa.Mfalme Fahd ameacha nyuma utawala wa kifalme unaolega lega huku miito ya demokrasia ikizidi kuhanikiza.Yaonyesha kana kwamba wakati umeanza kuwageukia wasuudia.

Gazeti la mjini Cologne,KÖLNISCHE RUNDSCHAU linaonya na kusema:

Pengine miaka kumi kutoa sasa Saud Arabia inaweza kugeuka janga jemngine la mivutano katika eneo la mashariki ya kati,ambako utajiri wake wa mafuta unazidi kutegemewa na mataifa kadhaa tajiri kwa viwanda.Kwamba mfalme Abdallah ameahidi angalao kwa sasa kufuata nyayo za mtangulizi wake,si hoja.Washington imeanza kuitambua hali hiyo tangu ilipogunduliwa kwamba wengi wa magaidi wa mashambulio ya september 11 mwaka 2001 ,walikua wasuudia-na ndio sababu pia ya kuongoza vita nchini Iraq.“

Maoni sawa na hayo yametolewa na gazeti la OFFENBURGER TAGEBLATT.Gazeti limeandika:

„Mizozo katika ghuba la uajemi ni mingi sawa na mchanga katika jangwa la bara arabu.Kwa kufariki dunia mfalme Fahd wa Saud Arabia,mzozo mwengine umechomoza.Hata kama Saud Arabia ni mshirika wa dhati wa Marekani na aliyeshika nafasi ya marehemu Fahd, mfalme Abdallah ni mpenda mageuzi, lakini muda sasa vichwa mchungu wa kihafidhina mjini Riyadh wamekua wakiotea kuung’owa madarakani utawala huo wa kifalme.Mwandani muaminifu wa jangwani anatishia kugeuka mtihani kwa nchi za magharibi.

Gazeti la mjini Berlin-BERLINER ZEITUNG limechambua kisa cha kuteuliwa John Bolton.

„George W. Bush anataka kwa kila hali kuzuwia thuluthi mbili ya sauti isipatikane katika kikao cha hadhara kuu ya umoja wa mataifa kuweza kuunga mkono mageuzi yaliyopendekezwa miongoni mwa wengineo na Ujerumani.Uamuzi wake umedhihirisha pia jinsi rais Bush alivyobanwa na wakati,miezi tisaa baada ya kuchaguliwa kwa kipindi cha pili madarakani.Ushawishi wake umeshaanza kudhoofika.Licha ya warepublican kudhibiti wingi wa viti katika mabaraza yote mawili ya Congress,rais anakabiliana na shida anapotaka kukamilisha malengo yake ya kisiasa.

Gazeti la mjini Bonn General Anzeiger limechambua msimamo wa Bolton kuelekea Umoja wa mataifa.Gazeti limeandika:

„Lawama za Bolton hazijalengwa kuuimarisha umoja wa mataifa.Kimsingi lawama zake si chochote chengine isipokua upinzani ulioshawishiwa na hisia kali za kizalendo.Akilinganishwa na John Bolton basi waziri wa ulinzi Donald Rumsfeld ni afadhali mara elfu.Bush anampendelea Bolton kwasababu ya umaarufu wake katika tawi la wahafidhina katika chama cha Republican.Kwa mtazamo wa vichwa mchungu wanaoelemea mrengo wa kulia chamani,umoja wa mataifa hauangaliwi kwa jicho jema.Na wanategemea kumuona balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa akitetea masilahi ya Marekani tuu.

Na hatimae mgomo wa madaktari nchini Ujerumani.Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linaonyesha kuyaelewa madai ya madaaktari hao.Linaandika:

„Hawalali wakapata usingizi wanapokua kazini usiku,masaa ya ziada yamerundikizana bila ya malipo-kazi nyingi ,mishahara kidogo na zaidi ya hayo,hata marupu rupu ya likizo yamefutwa na fedha za X-mas zinapunguzwa-wakipata fursa ya kuajiriwa nchi za nje,mtu anaweza kuwaelewa madaktari wa hospitali za Ujerumani wanapolazimika kufuata fedha.Maandamano yao yamelengwa zaidi dhidi ya siasa humu nchini.Wakulaumiwa hata hivyo kwa kupunguzwa mishahara ya madaktari wa hospitali ni wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi ambao kwasababu za kinadharia,wanapinga makubaliano ya maana kufikiwa.